.jpg)
Mkuu
wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Davis Mwamunyange akiwa katika ukumbi wa
Baraza la Uchumi la Umoja wa Mataifa maarufu kama ECOSOC ambapo ndipo
ulipofanyika mkutano wa kihistoria wa Wakuu wa Majeshi ya Ulinzi na
Maafisa wa ngazi za juu kutoka nchi zinazochangia katika Operesheni
za Ulinzi wa Amani chini ya Umoja wa Mataifa. Akichangia majadiliano ya
mkutano huo. Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi amelishauri Baraza Kuu la
Usalama na UN kuweka bayana na kwa uwazi mamlaka ya misheni
inazoziunda. Pamoja naye ni Brigedia Jenerali MG. Luwogo na Brigedia
Jenerali HS Kamunde.
.jpg)
Mkuu
wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyage akiwa ndani ya Ukumbi
Mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, akibadilishana mawazo na mmoja
wa Maafisa wa ngazi ya juu kutoka Idara ya Masuala ya Siasa katika UN
muda mfupi kabla ya Wakuu wa Majeshi ya Ulinzi hawajapiga picha ya
pamoja na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
.jpg)
Jenerali
Davis Mwamunyange akiwa na ujumbe wake katika picha hii ambayo wapiga
mbele ya bendera ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, muda mfupi baada
ya kumalizika kwa mkutano wa siku moja wa wakuu wa majeshi ya ulinzi
kutoka nchi 108 kutoka kushoto ni Kanal Adolf Mutta, Brigedia Jenerali
Luwogo, Mkuu wa Majeshi Jenerali Mwamunyange, Brigedia Jenerali
Kamunde, Meja Ngh'abi, na Luten Kanal Itang'are
.jpg)
"...Mnatuwakilisha
vema?" ndilo swali ambalo Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali
Mwamunyange alilowauliza watanzania hawa wawili, Afisa wa Usalama wa UN
Bw. Jacob Mwashiozya na Bw. Joseph Msami, wa Idhaa ya Kiswahili ya
Umoja wa Mataifa walipokuwa wakisalimiana naye na ujumbe wake mara
baada ya kumalizika kwa mkutano wa wakuu wa majeshi ya ulinzi
.jpg)
Katibu
Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, akiingia kwa staii ya aina yake
wakati alipokwenda kufungua mkutano wa kwanza wa aina yake kufanyika
katika Umoja wa Mataifa, ambapo Wakuu wa Majeshi ya ulinzi kutoka
nchi zaidi ya 100 walikutana kwa wakati mmoja na mahali pamoja
kujadiliana na kubadilishana mawazo kuhusu operesheni za ulinzi wa amani
za umoja wa mataifa.
Na Mwandishi Maalum, New York
Mkuu wa Majeshi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jenerali
Davis Mwamunyange, amelishauri Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa
Mataifa, kuweka bayana na kwa uwazi mamlaka ( mandate) ambayo
misheni ya kulinda Amani itapaswa kutelekeza kule inakopangiwa kwenda.
Ametoa ushauri huu siku ya Alhamisi wakati alipokuwa akitoa
mchango wake kwenye mkutano wa Wakuu wa Majeshi ya Ulinzi ambao nchi
zao zinachangia katika operesheni za ulinzi wa Amani za Umoja wa
Mataifa.
Katika mkutano huo uliokuwa wa siku moja, na kuhudhuriwa na
Wakuu wa Majeshi na Maafisa wa Ngazi za Juu ,kutoka nchi 108, Jenerali
Mwamunyage amesema;
“ Wakati wa utoaji wa idhini na mamlaka kwa misheni ya kulinda
Amani, Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa, linatakiwa kumwita
mbwa kwa jina lake kama lilivyo.Mbwa aitwe kwa jina lake. Elezeni
bayana na kwa uwazi mamlaka na idhini za utekelezaji za ya misheni
”
Na kuongeza, “ iwekwe wazi, kama ni misheni ya kulinda Amani, basi
ielezwe ni ya kulinda Amani, na kama ni ya matumizi ya nguvu basi na
iwe hivyo”. Amesisitiza Mkuu wa Majeshi
Amesema kwamba, kwa kutamka jina halisi /mamlaka ya misheni
pale inapoundwa, Baraza Kuu la Usalama linakuwa linapeleka ujumbe ulio
sahihi kwa pande zote zinazohusika pamoja na nini wakitarajie.
Jenerali Mwamunyage ameuleza washiriki wa mkutano huo mkutano wa
kwanza wa aina yake kuwakutanisha Wakuu wa Majeshi zaidi ya mia moja,
wakati mmoja na mahali pamoja. Kwamba, uwazi huo pia utasaidia kuweka
bayana hatua za utekelezaji zinazofanywa na walinzi wa amani kwenye
eneo la utekelezaji.
Vile vile Mkuu wa Majeshi ya Tanzania ameshauri pia kuwa misheni
ambayo tangu kuundwa kwake zilikuwa na mamlaka ya kutumia nguvu, ni
vema zisiendelee kutambuliwa hivyo pale mamlaka ya misheni hiyo
yanapobadilika kutoka matumizi ya nguvu na kuwa misheni ya kulinda
Amani au jina lolote lile.
Tanzania inawanajeshi wake katika Misheni mbalimbali ikiwa ni pamoja
na UNAMID ( Darfur) UNFIL, ( Lebanon) MONUSCO ( DRC) na katika maeneo
mengine.
Vile vile Tanzania ina Polisi na Askari Magereza ambao nao wanahudumu katika misheni mbalimbali.
Akizungumzia kuhusu mkutano huo ambao ulifunguliwa na Katibu Mkuu
wa Umoja wa Mataifa na Ban Ki Moon na kufungwa na Naibu Katibu Mkuu
Jan Eliasson. Jenerali Davis Mwamunyange amesema, mkutano kama huo
unapashwa kuitishwa mara kwa mara kwa kuwa unawawezesha wakuu wa
majeshi kubadilishana uzoefu wao katika utekelezaji wa operesheni za
ulinzi wa Amani na hasa kwa kuzingatia kwamba nchi wanachama ndio
wanaotoa wanajeshi wao na ndio haswa wanaokumbana na changamoto
mbalimbmali za utekelezaji wa dhamana hiyo.
Awali akifungua mkutano huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,
Ban Ki Moon pamoja na kuwashukuru Wakuu hao wa Majeshi kwa mchango wao
katika eneo hilo la ulinzi wa Amani, amesema operesheni ya kulinda
Amani chini ya Umoja wa Mataifa, licha kwa kwamba ni dhamana
inayohitajika sana lakini pia inakabiliwa na changamoto mbalimbali.
Akazitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni upugufu wa raslimali
fedha, zana, vifaa na teknolojia za kisasa lakini pia ugumu na hatari
wanazokumbana nazo walinzi wa Amani, ambapo hivi sasa mbinu za kigaidi
na uvamizi kwa walinzi wa Amani ni baadhi ya changamoto na hatari
wanazokumbana nazo.
Katibu Mkuu, amewataka wakuu hao wa majeshi kuongeza ushirikiano
wao kwa Umoja wa Mataifa na hasa katika kutafuta mbinu za kukabiliana
na changamoto za kiulinzi na kiusalama ambazo duni hivi sasa
inakabiliana nao.
Akaongeza kuwa kujitokeza kwa idadi kubwa ya wakuu hao wa majeshi ya
ulinzi kushiriki mkutano huo, kumeipa faraja kubwa Umoja wa Mataifa.
Naye Naibu Katibu Mkuu Jan Eliasson, akihitimisha mkutano huo,
amewataka wakuu hao wa majeshi na serikali zao kuendelea na majadiliano
ya mchakaTo wa kuundwa kwa majeshi ya ulinzi ya kikanda, majadiliano
ambayo yanatakiwa kuendelea kuelekea mkutano wa Operesheni ya Ulinzi
wa Amani utakaofanyika mwezi Septemba mwaka huu.
Wakuu hao wa Majeshi ya Ulinzi pamoja na kutoa mchango wa mawazo
yao, pia walipata fursa ya kupata maelezo kutoka kwa Viongozi wakuu
waandamizi wanaoongoza Idara zinazozohusu Operesheni ya Ulinzi wa
Amani.
habari kwa hisani ya MICHUZI BLOG