Naibu
Waziri wa Nishati na Madini (Nishati), Charles Mwijage (Kulia) akielekeza jambo
kwa baadhi ya Viongozi wa Kampuni ya Mafuta ya TIPPER alipotembelea Kampuni
hiyo hivi karibuni wakati wa ziara yake kwa Kampuni mbalimbali
zinazojishughulisha na biashara ya mafuta nchini.
Naibu
Waziri wa Nishati na Madini (Nishati), Charles Mwijage (Wa pili kutoka Kushoto)
akifuatana na baadhi ya Viongozi wa Kampuni ya Mafuta ya GAPCO kukagua
miundombinu ya kuhifadhia mafuta iliyoko eneo la Kampuni hiyo, Kurasini jijini
Dar es Salaam. Naibu Waziri alitembelea Kampuni mbalimbali zinazojishughulisha
na biashara ya mafuta nchini kufanya mazungumzo na kukagua miundombinu
inayotumiwa na Kampuni husika.
Meneja
wa Kampuni ya Mafuta ya HASS nchini Tanzania, Ali Hassan Ahmed (Kushoto),
akisikiliza maelekezo kutoka kwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini (Nishati),
Charles Mwijage (aliyeinua mkono) kuhusu utekelezaji wa mambo mbalimbali
unaotakiwa kufanywa na Kampuni hiyo, hususan kujenga mahusiano mema na jamii.
Wa kwanza Kulia ni Mbunge wa Temeke (Viti Maalum – CCM), Mariam Kisaka.
Joshua
Mtunda (mwenye Fulana ya Njano), akizungumza na Naibu Waziri wa Nishati na
Madini (Nishati), Charles Mwijage (wa Tatu kutoka Kushoto), kwa niaba ya Vijana
wenzake wanaofanya biashara ya kusafirisha abiria kwa Pikipiki/Bodaboda kuhusu
msaada wanaohitaji ili kuboresha biashara yao. Vijana hao wanafanya biashara
yao eneo la Kigamboni karibu na ilipo Kampuni ya Mafuta ya HASS.
Naibu
Waziri wa Nishati na Madini (Nishati), Charles Mwijage (wa kwanza – Kushoto),
akikagua miundombinu ya kuhifadhia mafuta ya Kampuni ya Mafuta ya PUMA katika
eneo la Kampuni hiyo, Kurasini jijini Dar es Salaam. Pamoja naye pichani ni
baadhi ya Viongozi wa Kampuni hiyo na Maafisa wa Serikali wanaoshughulikia
Sekta ya Mafuta.
Na Veronica Simba
Naibu
Waziri wa Nishati na Madini (Nishati), Charles Mwijage amezitaka Kampuni
zinazojishughulisha na biashara ya Mafuta nchini, kutumia mbinu mbalimbali za
kuboresha mahusiano mema na jamii zinazowazunguka ili kujenga imani kwa
wananchi na hivyo kupata ushirikiano katika masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja
na ulinzi wa miundombinu husika.
Aliyasema
hayo katika ziara yake hivi karibuni alipotembelea Kampuni mbalimbali za Mafuta
zilizoko jijini Dar es Salaam pamoja na kukagua miundombinu yao.
Mwijage
alisema, matatizo kama vile kuharibiwa kwa miundombinu ya kuhifadhia na
kusafirishia mafuta, pamoja na wizi wa mafuta unaofanywa na baadhi ya wananchi
unachangiwa na wananchi kutokuwa na imani na wafanyabiashara hao kwa kuwa
hawaoni manufaa ya moja kwa moja kwa jamii kutoka Kampuni hizo.
“Ikiwa
wananchi wataona manufaa ya uwepo wa Kampuni zenu katika maeneo yao, nina
uhakika watajenga imani kwenu na hawatakuwa tayari kuona mnaharibikiwa kwa
namna yoyote kwani wao pia watakuwa ni sehemu yenu,” alisema Mwijage.
Akifafanua
kuhusu namna nzuri ya kujenga mahusiano mema na jamii, Mwijage alisema inafaa
Kampuni hizo ziwasaidie wananchi kuinua vipato vyao kwa kuwapatia mitaji ya
fedha na vifaa vinavyohitajika kwa ajili ya biashara mbalimbali.
Naibu
Waziri alitoa mfano wa biashara ndogondogo za kusafirisha abiria kwa kutumia
Pikipiki maarufu kama Bodaboda zinazofanywa na vijana, pamoja na biashara ya
kuuza chakula maarufu kama Mama Lishe kwa akina mama na mabinti.
“Pamoja
na mambo mengine makubwa mnayosaidia jamii kama vile kuchangia elimu, nashauri
pia muone namna ya kusaidia mambo madogo madogo kama kuwanunulia bodaboda
vijana pamoja na kuwapa mitaji akina mama lishe,” alisisitiza Mwijage.
Aidha,
Mwijage alisisitiza Kampuni hizo kuwashirikisha Viongozi mbalimbali wa maeneo
husika wakiwamo Wabunge, Madiwani, Viongozi wa Kata na Mitaa husika katika
zoezi la kuainisha watu wanaohitaji misaada husika ili kuepuka utapeli kwa
kuwapatia wasio na sifa zinazostahili kupata misaada hiyo.
Katika
hatua nyingine, Naibu Waziri aliagiza Barabara ya Mafuta iliyoko eneo la
Mivinjeni-Kurasini jijini Dar es Salaam ifunguliwe ili kupunguza msongamano wa
magari unaochangia magari makubwa yanayosafirisha mafuta kwenda sehemu
mbalimbali nchini na nje ya nchi kutokusafiri kwa wakati hivyo kusababisha
hasara kwa Kampuni husika.
“Ninaomba
Halmashauri ya Manispaa ya Temeke iangalie uwezekano wa kuifungua njia hii
ambayo wameifunga, ili itumike kama ilivyokuwa ikitumika awali; magari yaingie
na kutoka kwa urahisi ili kuepusha msongamano uliopo,” alisisitiza Mwijage.
Naibu
Waziri alilazimika kutoa agizo hilo kufuatia hali ya msongamano mkubwa wa
magari aliojionea kwa baadhi ya Kampuni alizotembelea ikiwemo Kampuni ya GAPCO
iliyoko eneo la Kurasini.
Kwa
upande wao, wawakilishi wa Kampuni zilizotembelewa na Naibu Waziri, waliahidi
kuzingatia ushauri uliotolewa katika kuboresha mahusiano yao kwa jamii husika.
Na JIACHIE BLOG