BENKI
ya Posta Tanzania (TPB) Tawi la Mbeya, imetoa semina kwa Wajasiriamali
wa mkoa ikiwa na lengo la kuwaongezea ujuzi kwenye biashara zao. Semina
hiyo ya siku moja imefanyika kwenye ukumbi wa Mtenda Sunset mjini Mbeya
na kufunguliwa na Mkuu wa Wilaya, Profesa Norman Sigallah.
Akizungumza
kwenye uzinduzi wa semina hiyo ambayo pia ilihudhuriwa na Ofisa
Mtendaji Mkuu wa Benki ya Posta, Sabasaba Moshingi, Mkuu wa Wilaya
alitoa wito kwa wajisiriamali kutoogopa kukopa kwenye mabenki ili kukuza
mitaji yao na hatimae biashara zao.
Prof. Sigallah alitoa changamoto kwa wajasiriamali kuhakikisha biashara
zao zinaubora unaotakiwa ili kuweza kujenga imani na ushindani kwenye
soko. Mkuu huyo wa Wilaya alitoa changamoto kwa benki ya Posta kuweka
dawati maalum la wataalam watakaotoa ushauri kwa wajasiriamali pindi
wanapokuja kuomba mikopo.
Aliwashauri
wajasiriamali kujiepusha na makundi yenye muelekeo wa kuleta vurugu na
kuvunja amani, kwani ili kukua biashara yoyote inahitaji amani na
utulivi.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Posta, Sabasaba
Moshingi, akijibu maswali mbalimbali yaliyoulizwa na wajasiriamali hao
zaidi ya 150 waliohudhuria semina hiyo, alisema benki yake itaendelea
kuboresha huduma zake hasa upande wa mikopo, na pia kuangalia suala la
riba zinazotozwa kwa aina tofauti ya biashara.
"Benki yangu itaendelea kuangalia ni namna gani tunaweza kuweka wataalam
watakaotoa ushauri mzuri kwa wajasiriamali ili kupunguza mlolongo mrefu
wa nenda rudi kwa mkopaji.
Hii
ni katika jitihada za kuhakikisha kuwa mkopaji anapata mkopo kwa wakati
ili kuwahi fursa iliyojitokeza,".
Akiongea kwa niaba ya wajasiriamali hao, Bi. Joyce Mkongo, aliishukuru
sana benki ya Posta kwa kutoa mafunzo hayo kwao,ambayo yamewafungua
macho na kuwaondolewa woga wa kutumia huduma za kibenki. Alisema
wajasiriamali wengi wanasita kuchukua mikopo kwa hofu kuwa mali zao
zitataifishwa pindi watakaposhindwa kulipa mkopo.