.jpg)
Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda akizungumza na Bw. Witold Karczewski (kulia) ambaye
ni mmiliki wa kampuni ya Mlynpol ya Poland ambayo ina nia ya kujenga
maghala ya kisasa ya kuhifadhi nafaka katika kanda hapa nchini wakati
alipokagua maghala ya SGR mjini Dodoma Novemba 6, 2014
.jpg)
Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda akiongozana na Bw. Witold Karczewski (kulia)
ambaye ni mmiliki wa kampuni ya Mlynpol ya Poland ambayo ina nia ya
kujenga maghala ya kisasa ya kuhifadhi nafaka katika kanda hapa nchini
wakati alipokagua maghala ya SGR mjini Dodoma Novemba 6, 2014.
Picha na na habari
na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amekagua maghala ya kuhifadhia chakula yaliyopo
Kizota nje kidogo ya mji wa Dodoma ikiwa ni utekelezaji wa ahadi
aliyoitoa Alhamisi iliyopita kwamba Serikali inalenga kujenga maghala
kwenye mikoa sita kupitia mkopo ambao itaupata kutoka Serikali ya
Poland.
Akizungumza
na viongozi wa mkoa wa Dodoma pamoja na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya
Chakula (NFRA) leo asubuhi (Alhamisi, Novemba 6, 2014) wakati akikagua
maghala hayo, Waziri Mkuu alisema katika mkoa huo, Serikali ina nia ya
kujenga maghala makubwa (SILOS) yenye uwezo wa kuhifadhi tani 100,000 za
nafaka kwa wakati mmoja.
“Tukipata
maghala yenye uwezo wa kuhifadhi tani 100,000 tutakuwa na uhakika wa
kuchukua na akiba ya nafaka kutoka mikoa ya jirani ya Singida, Tabora na
Manyara,” alisema.
Waziri Mkuu alifuatana na Bw. WITOLD KARCZEWSKI ambaye ni mmiliki
wa kiwanda kikubwa cha kusindika nafaka nchini Poland ambacho Waziri
Mkuu Pinda alikitembelea alipozuru nchi hiyo Oktoba 24, mwaka huu. Bw.
KARCZEWSKI anamiliki pia kiwanda kinachotengeneza malighafi za kujengea
SILOS.
Akitoa
taarifa mbele ya Waziri Mkuu, Mkuu wa kituo cha NFRA Kanda ya Kati, Bw.
Ruwaichi Mambali alisema kituo hicho kina maghala yenye uwezo wa
kuhifadhi tani 30,000 lakini kwa sasa kina tani 69,000 ambazo kati ya
hizo tani 62,000 zipo Kizota (Dodoma) na tani 7,000 ziko Manyoni
(Singida).
Alisema
eneo zima la Kizota lina ukubwa ekari 33 na kwamba kuna maghala matatu
yenye uwezo wa kuhifadhi tani 10,000 kila moja. “Lakini kwa sasa
tumelazimika kuweka mahindi mengine na mtama hapa nje ambayo
tumeyafunika kwa maturubali,” alisema.
Kwa
upande wake, Bw. KARCZEWSKI alitaka kufahamu miundombinu iliyopo kwenye
ghala la Kiszota ikiwemo umabli wa kutoka barabara kuu pamoja na reli.
Pia alitaka kujua eneo zima lina ukubwa kiasi gani. Na alitaka kufahamu
mbinu zinazotumika hivi sasa kuhifadhi chakula kwenye ghala hilo.
Alisema
wakipata michoro ya eneo hilo (site map), atatuma wataalamu wake
Januari mwakani waangalie uwezekano wa kuanza ujenzi mapema iwezekanavyo
pindi mazungumzo yakikamilika.
Alhamisi
iliyopita, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es
Salaam mara baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Mwl. Julius
Nyerere akitokea Oman, Waziri Mkuu alisema alikwenda Poland kutafuta
msaada wa mfumo wa mkopo wenye masharti nafuu ambao utasaidia kupambana
na tatizo la uhaba wa maghala kwa ajili ya kuhifadhia nafaka.
Alisema
Serikali imelenga mikoa sita ya kuanzia ambayo ni Ruvuma, Rukwa, Njombe
(pamoja na Iringa) ambako kuna uzalishaji mkubwa wa mahindi. Pia
inaangalia Kanda ya Ziwa ambako mara nyingi wana uhaba wa chakula; na
kwamba itaweka maghala mkoani Dodoma kwa sababu ni katikati ya nchi ili
ikusanye akiba kutoka mikoa ya jirani ya Singida, Manyara na Tabora.
“Lengo
ni kupata uwezo wa kuhifadhi tani 700,000 hadi 1,000,000 na ujenzi wao
siyo kama huu wa kwetu. Tumewaomba watujengee SILOS (maghala makubwa)
kwa sababu zina teknolojia ya kujua kiasi gani cha nafaka kimeingia,
zina unyevu kiasi gani, unaweza kuweka dawa nafaka zako, kuosha na
kukausha na kisha ukasindika kwa kiwango unachotaka,” Waziri Mkuu
aliwaeleza waandishi wa habari.
Alisema
uzalishaji mwaka huu umetoa ziada ya tani milioni 1.5 za nafaka na tani
800,000 za mpunga ikilinganishwa na ziada ya tani 300,000 iliyokuwepo
mwaka jana. “Serikali inakabiliwa na changamoto ya kupata soko la
uhakika kwa mazao ya wakulima kwa sababu tulizoea kumtumia Wakala wa
Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA) kama mnununzi mkuu na uwezo wezo wake
ni tani 240,000 tu kwa mwaka,” alisemaHABARI NA MICHUZI BLOG