
Migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji imeendelea kusababisha mauaji wilayani Kiteto mkoani Manyara baada ya watu watano, wakiwamo wakulima watatu na wafugaji wawili, kuuawa.
Mauaji
hayo yalitokea juzi na jana kwenye vijiji vya Kazinguru na Lamrambogo
katika Kata ya Matui ambako watu zaidi ya kumi na mmoja wanadaiwa
kujeruhiwa huku maboma 14 ya wafugaji yakichomwa moto na wakulima na
mifugo kadhaa kuuawa.
Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo
waliokuwa kwenye Zahanati ya Matui jana wakisubiri miili ya marehemu na
majeruhi wa vurugu hizo, walidai chanzo cha mauaji hayo ni kifo cha
mkulima mmoja aliyeshambuliwa na wafugaji.
Mmoja kati
ya mashuhuda hao, Mbwana Juma alisema mkulima huyo alikuta mifugo
imeingia shambani kwake na kula mihogo, na alipouliza jambo hilo,
wafugaji wakamkatakata na kumuua.
Alisema baada ya
wakulima kupata taarifa ya kuuawa kwa mwenzao, ndipo walipochukua silaha
za jadi na kuwaua wafugaji wawili, mwanamke na mwanaume na kukamata
mifugo ambayo waliichinja na kula nyama.
Alisema baada
ya wafugaji kuona wenzao wameuawa kwa mapanga na sime, ndipo baadhi yao
walipochukua silaha za baridi na za moto ikiwamo bunduki na kuwaua
wakulima wanne. Kuna hofu kuwa maiti zaidi zzipo eneo hilo.
Alisema
hadi jana jioni, hali ilikuwa tete eneo la Matui na maduka yalikuwa
yamefungwa huku shughuli zote zikiwa zimesimama kwa hofu ya vurugu.
Kamanda
wa polisi wa Mkoa wa Manyara, SACP Deusdedit Nsimeki, akizungumza kwa
njia ya simu jana jioni, alithibitisha kuuawa kwa watu watano kwenye
eneo hilo la Matui.
Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Martha
Umbulla alisema kwa njia ya simu wakati akielekea eneo la tukio kuwa
hajapewa taarifa ya idadi kamili ya watu waliouawa