
KAMPUNI ya simu ya Viettel ya Vietnam inayokua kwa kasi duniani ambayo sasa inahamishia nguvu zake katika soko la Tanzania, imetangaza ajira kwa wasomi wa Tanzania zaidi ya 2,000.
Viettel
ambayo uongozi wake wa juu ulikutana na Rais Jakaya Kikwete akiwa
ziarani nchini Vietnam hivi karibuni na kuahidi kufanya mapinduzi
makubwa katika sekta ya mawasiliano nchini, imetangaza nafasi hizo
kupitia gazeti la Habari Leo na Daily News matoleo ya jana.
Kwa
mujibu wa tangazo hilo, Viettel inahitaji wataalamu wa karibu fani
zote, huku kiwango cha chini kabisa cha elimu kikiwa stashahada, yaani
diploma.
Wafanyakazi
wanaohitajika ni wenye ujuzi katika masuala ya rasilimaliwatu, sheria,
fedha, uhasibu, masoko, uchumi, mipango, takwimu, uwekezaji, ugavi,
usafirishaji, utunzaji wa vifaa, umeme, simu, teknolojia ya habari na
mawasiliano, biashara, utawala na uhusiano wa umma.
Tangazo
hilo limeendelea kuonesha kuwa, waombaji wanatakiwa kutuma maombi yao
kuanzia leo kwa njia ya baruapepe, mwombaji akitakiwa kutuma ujumbe
unaoomba fomu kupitia anuani za makao makuu na pia mameneja wa kampuni
hiyo walioko katika mikoa yote, Tanzania Bara na Zanzibar.
Moja
ya anuani ya makao makuu inasomeka; viettelrecruiter@ gmail.com, ambapo
mtumaji baada ya kuwasilisha ombi lake, atatumiwa fomu maalumu.
Mwenyekiti
wa Viettel inayomilikiwa na Jeshi la Vietnam, Nguyen Manh Hung katika
mazungumzo yake na Rais Kikwete, alisema kampuni yake inakusudia kuja na
huduma bora zitakazomwezesha kila Mtanzania kumiliki simu ya kisasa
(Smart phone), kutokana na punguzo kubwa la bei, licha ya ubora wa
huduma zake.
Aidha,
aliahidi Viettel itafunga huduma ya mawasiliano ya intaneti katika kila
kijiji nchini, huku taasisi za umma kama vile shule, hospitali, vituo
vya Polisi vikinufaika kwa kupatiwa huduma hiyo bila malipo yoyote.
Kwa
mujibu wa Hung, kampuni yake inapanga kupunguza bei ya simu za kawaida
hadi kufikia dola za Marekani 15, sawa na Sh 25,000 na kupunguza bei ya
smart phone hadi kufikia dola za Marekani 40, sawa na Sh 65,000.
Sasa hivi, bei ya simu hizo ni kubwa zaidi ya kiasi hicho kinachokusudiwa.
Mwenyekiti
huyo aliongeza kuwa, kampuni yake itawekeza kiasi cha dola za Marekani
bilioni moja (Sh trilioni 1.7) katika huduma za simu na huduma nyingine
nchini Tanzania, hivyo kuifanya Tanzania kuwa nchi ya pili nyuma ya Peru
kupata mfumo wa simu wa kisasa zaidi miongoni mwa nchi ambako kampuni
hiyo ina shughuli zake.
Alisema
ndani ya miaka mitatu tangu kampuni hiyo kuanza shughuli zake nchini,
kiasi cha vijiji 4,000 ambavyo kwa sasa havina mawasiliano, vitapatiwa
huduma hiyo katika awamu ya kwanza.