Jaji Warioba
Rasimu ya
Katiba inayopendekezwa iliyowasilishwa bungeni juzi, imeondoa Ibara 28
zikiwamo zinazowataka viongozi wa umma kutopokea zawadi kwa manufaa yao
binafsi wala kufungua akaunti ya benki nje ya nchi pasipo sababu
maalumu, Mwananchi limebaini.
Ibara ya
15 iliyokuwamo katika Rasimu ya Warioba ilisema: "Kiongozi wa
umma
wakati anapotekeleza shughuli za kiserikali, akipewa zawadi, zawadi hiyo
itakuwa ni mali ya Jamhuri ya Muungano na ilitaka Bunge kutunga sheria
itakayosimamia, pamoja na mambo mengine, thamani, kiwango, aina na
uhifadhi wa zawadi kwa Jamhuri ya Muungano. Mbali na ibara hiyo, pia
Ibara ya 16 iliyohusu ufunguaji akaunti nje ya nchi, imeondolewa.
Ibara
nyingine zilizoondolewa ni pamoja na ya 17 iliyopendekeza uwazi wa mali
ikimtaka kiongozi wa umma kutangaza thamani ya mali na madeni yake mara
tu baada ya kupata uongozi.
Pia Ibara
ya 129 iliyokuwa inawaruhusu wananchi kumvua madaraka mbunge ambaye
atashindwa kuwasilisha au kutetea kwa dhati hoja zinazotokana na kero za
wapigakura wake au ataacha kuishi au kuhamisha makazi yake kutoka eneo
la jimbo la uchaguzi kwa zaidi ya miezi sita bila sababu za msingi
imeondolewa.
Ibara 28 zilizoondolewa
15. (1)
Kiongozi wa umma wakati anapotekeleza shughuli za kiserikali, akipewa
zawadi, itakuwa ni mali ya Jamhuri ya Muungano na ataiwasilisha kwa
Katibu Mkuu Kiongozi kupitia kwa katibu mkuu wa wizara au kiongozi wa
taasisi ya Serikali inayohusika, akiainisha:(P.T)
(a) aina ya zawadi; (b) thamani ya zawadi; (c) sababu ya kupewa zawadi; na (d) mtu au mamlaka iliyotoa zawadi hiyo.
(2) Neno
"zawadi" kama lilivyotumika katika ibara hii linajumuisha kitu chochote
chenye thamani atakachopewa kiongozi wa umma katika utekelezaji wa
shughuli za umma.
(3) Bunge
litatunga sheria itakayosimamia, pamoja na mambo mengine, thamani,
kiwango, aina na uhifadhi wa zawadi kwa Jamhuri ya Muungano.
16. Kiongozi wa umma-
(a)
Hatafungua au kumiliki akaunti ya benki nje ya Jamhuri ya Muungano
isipokuwa tu kwa namna ambayo sheria za nchi zinaruhusu; na (b) hataomba
au kupokea mkopo au faida yoyote kwa namna au mazingira ambayo
yanashusha hadhi au heshima ya utumishi wa umma.
17.-(1)
Kiongozi wa umma atalazimika kutangaza na kuwasilisha, ndani ya siku
thelathini baada ya kupata uongozi na baada ya kuacha uongozi, mali na
thamani yake na madeni yake katika Tume ya Maadili ya Uongozi na
Uwajibikaji.
Chanzo:Mwananchi