Akizungumza
na Mikito Nusunusu, mratibu wa tamasha hilo, Luqman Maloto alisema kila
kitu kimekwenda kwenye mstari na kinachosubiriwa ni muda ufike,
Watanzania wajumuike kwa pamoja uwanjani kushuhudia burudani zisizo na
mfano.
Kwenye
muziki wa Injili, Maloto alisema mkongwe wa nyimbo za Injili, Upendo
Nkone ataliongoza jukwaa kwa kuporomosha nyimbo kama Haleluya Usifiwe,
Mwambie Yesu, Unastahili Kuabudiwa, Usinipite Bwana na nyingine nyingi.
Kama
hiyo haitoshi, watakuwepo Martha Mwaipaja anayetamba na wimbo wa
Tusikate Tamaa na Ombi Langu, pia katika kundi hilo wapo Ambwene
Mwasongwe, Angela na Paul Clement. Katika kuleta raha zaidi, Maloto
alisema mgeni rasmi safari hii atakuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Dk. Mohamed Gharib Bilal. “Dk. Bilal ndiye
atakayepuliza kipyenga kuanza kwa mechi kati ya Wabunge Mashabiki wa
Simba dhidi ya wenzao wa Yanga.”
Kwa
upande wa Wabunge wa Yanga imefanya usajili wa nguvu kwa kumchukuwa,
Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Jakaya Kikwete wakati Simba wamefanikiwa
kumsajili, Mbunge wa Kalenga, Godfrey Mgimwa
Pia viongozi mbalimbali wa kitaifa, wakiwemo mawaziri na mabalozi wanaowakilisha nchi mbalimbali hapa nchini, wanatarajiwa kuhudhuria tamasha hilo na kuandika historia kwa pamoja.
Maloto
amesema kutakuwa na mpambano mkali kati ya bondia anayeshikilia mkanda
wa UBO, Thomas Mashali dhidi ya Mada Maugo ambaye hajawahi kumpiga
mwenzake huyo katika pambano lao lilofanyika mara ya mwisho.
“Mashabiki
wajitokeze kwa wingi kuja kumuona mkali wa muziki wa dansi, Khalid
Chokoraa akizichapa dhidi ya Said Memba huku mastaa wa Bongo Movie Jacob
Steven ‘JB’ akizitwanga na Cloud 112.” Ndondi nyingine za kukata na
shoka ni pale Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba atakapozichapa
ulingoni na Mbunge wa Nzega, Dk. Hamis Kigwangala.
Maloto
aliongeza kuwa kutakuwa na mechi kali za mpira wa miguu ambapo Azam FC
itaumana vikali na Mtibwa Sugar.Kama hiyo haitoshi, Bongo Movie
watakipiga na Bongo Fleva. Akasema burudani haitaishia hapo, kwani
mastaa kibao wa Bongo Fleva watakuwepo kupiga shoo baab’kubwa.
“Tutakuwa
na mfalme wa Bongo Fleva, Ali Kiba. Mashabiki wategemee kusikia nyimbo
zake zote kali sambamba na hizi mpya za Kimasomaso na Mwana.”Mastaa
wengine watakaolipamba jukwaa siku hiyo ni pamoja na Madee, Meninah,
Scorpion Girls, R.O.M.A, Nyandu Tozi, Navy Kenzo, P-Plan, Shilole, Juma
Nature na kundi zima la TMK Wanaume Halisi.
Tamasha
la Usiku wa Matumaini limedhaminiwa na Vodacom, Pepsi, PSI, Benki ya
Posta, GEPF, Azam TV, E.FM (93.7), Gazeti la Championi, Times FM
(100.5), SYSCORP na Clouds FM/TV.