
Aliyekuwa
msajili wa vyama vya siasa nchini, John Tendwa amesema Rais Jakaya
Kikwete aliteleza kueleza msimamo wake na ambao baadaye ulibainika kuwa
wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wakati akizindua Bunge Maalumu la Katiba,
Machi 21.
Tendwa,
ambaye alistaafu Agosti mwaka jana na nafasi yake kuchukuliwa na Jaji
Francis Mutungi, alitoa kauli hiyo jana katika mahojiano maalumu na
Mwananchi ofisini kwake jijini Dar es Salaam.
Tendwa,
ambaye alikuwa Msajili kwa miaka 13, alisema akiwa kiongozi mkuu, Rais
Kikwete alipaswa kutoa mwongozo wa uendeshaji wa Bunge Maalum la Katiba.(P.T)
"Sikuwapo
nchini, lakini kwa kadri ninavyoelezwa, kama hiyo ni kauli yake, basi
alijisahau kusemea msimamo wa chama chake, (CCM) na sera yake ya
serikali mbili katika bunge hilo," alisema.
"Rais ni
mtendaji, alipaswa kutoa guidelines (miongozo) ya jinsi ambavyo Bunge
Maalum la Katiba linatakiwa kufanya. Alichokisema, aliteleza.
"Alijisahau na kurudi kwenye chama kwa sababu hiyo ndiyo sera ya chama chake, " alisema Tendwa.
"Na siyo
yeye tu (Kikwete) kwani nimemsikia hata Dk Shein (Rais wa Zanzibar na
mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi), akisema kuwa msimamo wa CCM ni
serikali mbili," aliongeza Tendwa.
"Nimemsikia
Makamu wa Pili wa Rais (Balozi Seif Ali Iddi) akisema hivyo na Rais
wangu (Kikwete) katika mikutano mbalimbali ya hadhara, naye amelisema
hilo."
Madai ya kuibeba CCM
Tendwa
ambaye katika uongozi wake wa miaka 13 alikuwa akituhumiwa mara kwa mara
na vyama vya upinzani kuwa anakibeba chama tawala, alisema: "Nadhani na
yeye (Rais Kikwete) kasema. Nadhani alijisahau kuwa ni kiongozi wa
taifa."
"Rais ni mtendaji na mimi nasema aliteleza. Turudi katika hoja kwa kujadili rasimu iliyoko mezani."
Kauli
hiyo imekuja kipindi ambacho baadhi ya viongozi wakiwamo wa vyama vya
siasa nchini, Dk Wilbroad Slaa (Chadema), Makamu wa Kwanza wa Rais
Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad na pia aliyekuwa mwenyekiti wa Tume
ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, pia kumkosoa Rais Kikwete.