Hebu
jaribu kuvuta picha katika ubongo wako, waheshimiwa wabunge
watakapoweka kando masuala ya ‘Ukawa’ na ‘Tanzania Kwanza’, kisha
kukutana katika uwanja kuonyeshana umwamba kwa kusakata gozi la ng’ombe
katika mchezo huu wa kihistoria.
Kila
timu tayari imeingia mafichoni kujiwinda na mchezo huo ili kuhakikisha
inaibuka kidedea na kujenga heshima mbele ya watani wao huku Simba
wakiahidi kulipiza kisago cha bao 1-0 walichokipata mwaka jana kutoka
kwa Yanga. “Tayari tumeingia kambini kujiwinda na mchezo huu ili kuziba
midomo na kelele za Yanga ambao wamekuwa wakitamba tangu watubahatishe
mwaka jana,” alijinasibu Hamis Kigwangala ambaye ndiye nahodha wa Simba.
Kwa
upande wa mlezi wa Yanga ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Temeke,
Abassi Mtemvu, alijigamba kuwa ni lazima waendeleze moto wa ushindi kwa
kuwa wapo na kikosi imara na tayari wameshaingia kambini kwa kuwa mchezo
huu ni siriazi kwao.
“Kwa
kweli mchezo huu tumeuchukulia kwa mtazamo wa juu kabisa na lazima
tuwapige kwa kuwa tuna damu changa nyingi, hatuna masihara, maana
wakitufunga hatutakaa bungeni. “Tupo katika maandalizi ya mwisho kwa
sasa ingawa tulipoweka kambi yetu itabaki kuwa siri,” alisema Mtemvu
kwa kujiamini.
Baadhi
ya wabunge wanaounda timu ya Yanga ni pamoja na Abassi Mtemvu,
Ridhiwani Kikwete, Freeman Mbowe na Mwigulu Nchemba, huku kikosi cha
Simba kikiundwa na wakali kama Zitto Kabwe, Hamisi Kigwangalla, Wiliam
Ngeleja, Juma Nkamia, Amos Makalla na Ismail Aden Rage. Mbali na mchezo
huo ambao utakuwa kivutio kikubwa kwa wadau wa soka, pia kutakuwa na
mchezo mwingine wa kusisimua pale Bongo Fleva chini ya mkali wao, Peter
Manyika itakapopepetana na Bongo Movie FC chini ya Jacob Steven JB.
Mkurugenzi
wa Ufundi wa Bongo Movie, Fatuma Makongoro ‘Bi Mwenda’, tayari ameanika
wachezaji wake huku akisema kuwa hahofii kwani kikosi chake kipo
kamiligado kuelekea mchezo huo ambao wameuchukulia kwa umakini mkubwa.
*
“Sisi
tumeuchukulia ‘serious’ sana mchezo huu kwa kuwa mashabiki wetu
watakuja wengi na hatutakubali kuwaangusha.“Wachezaji waliopo kambini
mpaka sasa ni Mzee Majuto, Kingwendu, Bambo, JB, Steve Nyerere, Dk
Cheni, Ray, Mtitu, Cloud pamoja na Muhogo Mchungu,” alisema Bi Mwenda.
Akijibu
mapigo ya wapinzani wao, kocha wa Bongo Fleva ambaye pia anakinoa
kikosi cha Yanga, Juma Pondamali ‘Mensah’, alisema Bongo Movie wajiandae
kupata kipigo cha mshangao kwa kuwa wao hawatakwenda kuigiza uwanjani.
“Hawa
waigizaji wajiandae na kipigo cha ‘sapraizi’, maana pale sisi hatuendi
kuigiza, tunaenda kupiga kazi kwa kuwa mpira hauigizwi, unachezwa kila
mmoja anaona, sasa acha wapige domo wataona kitakachowakuta,” alisema
Pondamali. Baadhi ya mastaa wanaounda kikosi cha Bongo Fleva ni pamoja
na Peter Manyika, H-Baba, Ali Kiba, Rich One, Kalapina na wengineo.
Ukiachana
na soka, pia kutakuwa na burudani mbalimbali ambapo mastaa kibao kutoka
ndani na nje ya nchi watakuwepo kulipamba jukwaa la Usiku wa Matumaini.
Baadhi ya mastaa hao ni pamoja na Yemi Alade kutoka Nigeria, Madee, Ali
Kiba, Roma Mkatoliki, Shilole, Menninah, Juma Nature na kundi zima la
TMK Wanaume Halisi.
Mgeni
rasmi katika tamasha hili atakuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Dk Mohammed Gharib Bilal.Tamasha la Usiku wa Matumaini
limedhaminiwa na Clouds FM (88.5), Times Fm (100.5), Vodacom, Pepsi,
Azam TV pamoja na Syscorp.