Na Nassoro Gallu
UNAPOZUNGUMZIA Nigeria katika ulimwengu wa muziki kwa sasa unazungumzia levo nyingine, jina la Yemi Alade ni moja ya majina ‘hot’, mdada anayemiliki jina hilo anajua kudansi, anajua kucheza na jukwaa, ni mkali wa sauti, mcheshi, vyote hivyo vinampa nafasi ya kutamba.
Mratibu wa tamasha hilo, Luqman Maloto amesema mdada huyo ambaye kimuonekano anavutia amewasiliana na waratibu na kuwaahidi kuwa lazima atampata Johnny wake ndani ya ardhi ya Uwanja wa Taifa.
“Yemi hakuwa na jina kubwa lakini tangu alipotoa wimbo wake huo, nadhani hakuna Mtanzania mpenda burudani ambaye hajui kuhusu wimbo huo, kila kitu kinaenda vizuri na watu wajiandae kwa shoo kali zaidi ya miaka iliyopita.
“Tamasha la Matumaini limejitengenezea heshima kubwa tangu lilivyoanza, hivyo tunawaahidi Watanzania kuendeleza imani yao hiyo kwa kufanya mambo makubwa,” alisema Maloto.
Upande wa Yemi ambaye alianza kuliona jua mwaka 1989, alianza muziki ‘serious’ mwaka 2005 ambapo alikuwa kiongozi wa Kundi la Noty Spices. Baadaye akashiriki katika shindano la vipaji la Peak mwaka 2009 na kuwa mshindi.
Baadaye alitoa singo ya Fimisile, Ghen Ghen kisha Johnny na sasa anatamba na Tangerine aliomshirikisha Selebobo, pia yupo kwenye maandalizi ya albamu yake ijayo aliyoipa jina la King of Queens.
Utamu mwingine wa Tamasha la Matumaini
Mada Maugo Vs Thomas Mashali
MASHALI ambaye anashikilia mkanda wa UBO na Bingwa wa Afrika Mashariki na Kati ameahidi kumfanyia mbaya Maugo na kusema lazima amfanyie kitu kibaya ulingoni, lakini Maugo naye amejibu kwa kusema atazing’oa rasta za Mashali kwa mikono yake mwenyewe.
Mara ya mwisho walitwangana Agosti 30, 2013, Mashali akashinda katika raundi ya 10. Safari hii kazi ipo!
Wabunge Yanga Vs Simba
WABUNGE wa Yanga wanajinasibu kwa usajili mpya wa Ridhiwan Kikwete wakati wenzao wa Simba wamemsajili straika hatari Godfrey Mgimwa. Mwaka jana, Yanga walishinda kwa bao 1-0, safari hii Simba wamesema watafia uwanjani lakini siyo kufungwa na wapinzani wao hao.
Bongo Movie Vs Bongo Fleva
NAHODHA wa Bongo Movie, Steve Nyerere ameshaweka wazi kuwa kamati yao ya ufundi chini ya Bi Mwenda imeshamaliza kila kitu wakati upande wa Bongo Fleva wao wamedai kuwa wapo chimbo wakijifua.