BABA wa
mwanafunzi aliyefanya vizuri katika mtihani wa kidato cha sita na
kushika nafasi ya pili kitaifa masomo ya sayansi, Doris Noah amesema
mtoto wake ana ndoto ya kuwa rubani lakini bado hakubaliani na maamuzi
yake.
Akizungumza
katika chumba cha habari cha gazeti hili jana, Noah Odiero ambaye ni
Mshauri na Mlezi wa Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma, amesema binafsi
amefurahishwa na matokeo ya mtoto wake.
Hata
hivyo alisema alikuwa akimshauri kusomea masuala ya uhandisi wa migodi
na petroli, lakini matokeo yametoka sasa hivi tutaona tuchague nini.(MM)
“Tanzania bado sana kwa taaluma hii nchi yenyewe haina ndege anaweza tu kupoteza taaluma yake,” alisema.
Akijibu swali nini anadhani siri ya ushindi kwa mwanae alisema ni kujisomea na kupenda kusali.
“Namshukuru
Mungu nimefurahi kwa mwanangu kufanya vizuri, lakini mpaka sasa
sijaongea na mwanangu kwani sasa yuko kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa
JKT Kanembo Kigoma walivyofika kule wamenyang’anywa simu, sikuongea naye
kwa vile nilikuwa nimeongea na afande labda atakuwa amemuambia,”
alisema.
Alisema
Doris ni mtoto mpole hasa akiwa nyumbani kama akiwa hana shughuli
atakuwa nyumbani amepumzika na mara nyingi anapenda kujisomea vitabu.
Pia alisema anapenda sana kusali na kitu kingine anachoamini kumsaidia mwanawe kufanya vizuri ni kukubaliana na matakwa yake.
Alisema
Doris alizaliwa Julai 29, mwaka 1995 katika hospitali ya Muhimbili
Jijini Dar es Salaam na alisoma darasa la kwanza katika shule ya msingi
Segerea ambapo baadaye shule hiyo ikagawanywa na kuwa shule mbili za
Segerea na Maendeleo.
Alisema
Doris alihamia Maendeleo akiwa darasa la tano na alimaliza darasa la
saba ambapo alifaulu na kupangiwa kwenda shule ya wasichana ya Kisutu.
Alisema
wakati akisoma shule ya msingi alikuwa akishika nafasi za juu lakini
licha ya kufaulu kwenda Kisutu aliomba asipelekwe Kisutu kutokana na
matatizo ya usafiri na shida ya kuamka asubuhi.
Alisema
aliamua kumtafutia mtoto wake shule ya bweni katika Wilaya ya Same
Mkoani Kilimanjaro kwenye shule ya Sekondari ya wasichana ya Kandoto
ambapo alisoma kidato cha kwanza kuanzia mwaka 2008 hadi 2011.
Odiero
alisema kwenye mtihani wa kidato cha nne alipata daraja la kwanza pointi
nane na kuwa wanafunzi kumi bora kitaifa. Odiero mwenye watoto wanne,
anasema mkewe ni Neema Kidela ambaye ni mwalimu katika shule ya Msingi
Ipagala B, Dodoma