NAIBU Katibu Mkuu wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), *Zitto
Kabwe amesema kuwa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania analipwa sh
milioni 384 kwa mwaka,
sawa na sh milioni 32 kwa mwezi pasipo kukatwa kodi.*
Hii ni mara ya pili
kwa Zitto kutangaza hadharani mishahara ya viongozi
wakuu wa serikali,
akiwa ameanza na ule wa Waziri Mkuu, aliyesema
analipwa takribani sh
milioni 26 kwa mwezi.
Akiwahutubia wananchi
mjini Igunga jana, ukiwa ni mwendelezo wa ziara
yake ya kuimarisha
chama Kanda ya Magharibi, Zitto ambaye pia ni mbunge
wa Kigoma Kaskazini
alisema kuwa sababu ya kutaka mishahara ya viongozi
wakuu wa nchi
ijulikane, ni kuzuia mianya ya watu wachache kuiibia nchi
kutokana na usiri wa
jambo hilo.
Zitto alisema hoja ya
msingi si kiasi wanacholipwa viongozi hao
walioajiriwa na
wananchi, bali ni usiri unaofanywa juu ya kiwango hicho
jambo alilosema kuwa
linaweza kutumiwa na wajanja kuendelea kuinyonya nchi.
Alisema ni jambo la
kusikitisha kuona mwalimu anayelipwa mshahara wa sh
220,000 kwa mwezi
akikatwa kodi, huku viongozi wa kuchaguliwa wakiwa
wanapokea mishahara
mikubwa pasipo kukatwa kodi licha ya kuhudumiwa kila
kitu na serikali.
Aliongeza kuwa katiba
ya sasa Ibara ya 43(1), inaeleza kuwa rais
atalipwa mshahara
pamoja na malipo mengine, huku ibara hiyo hiyo kifungu
cha pili ikizuia
mshahara na marupurupu kupunguzwa, hali aliyoelezea
kuwa ni muhimu katiba
mpya ikabadilisha sheria hizo kwa manufaa ya nchi.
“Kwa hiyo hata kesho
kama Dk. Willibrod Slaa akiwa rais na akataka
kupunguza mshahara
wake, kwa katiba hii hawezi na hili jambo si sahihi
kwani viongozi wa
ngazi hizi wanapata kila kitu bure kutoka serikalini,”
alisema Zitto.
Akiwa katika Kata ya
Choma, Zitto alikagua kilichokuwa kiwanda cha
kuchambulia pamba cha
Giner ambacho kimeacha kufanya kazi tangu mwaka 1998.
Alisema kufa kwa
viwanda vingi vya uzalishaji nchini kumechangiwa kwa
kiasi kikubwa na
Serikali ya Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin
Mkapa, akidai kuwa
alishindwa kutofautisha suala la uwekezaji na
biashara huru.
“Ni serikali ya Mkapa
ndiyo ilitufikisha hapa katika kupotea kwa viwanda
nchini, wao walidhani
biashara huru ni kuwapa wawekezaji viwanda vyetu
na serikali kujiweka
pembeni, sasa nchi imebaki kutegemea uchumi wa
uchuuzi badala ya
uzalishaji,” alisema.
Alisema sera ya
uwekezaji katika Serikali ya CCM ilichukuliwa kama fursa
ya viongozi wa chama
hicho kujinufaisha na mali za serikali pasipo kujua
wataendeleza vipi.
Zitto alisisitiza kuwa
kila mara CHADEMA imekuwa ikisisitiza bungeni juu
ya kupiga marufuku
usafirishaji wa pamba kwenda nje kama malighafi, na
badala yake wakitaka
viwanda vifufuliwe kwa ajili ya kutoa ajira kwa
Watanzania.
Alirejea kusisitiza
sera ya hifadhi ya jamii kwa wakulima akisema
imefikia wakati
serikali kupitia SSRA ione umuhimu na ulazima wa
kuhakikisha wanaongeza
Watanzania wenye hifadhi ya jamii kwa kuanza
mfumo maalumu wa
hifadhi ya jamii kwa wakulima (Supplementary scheme for
social security to
small holder farmers).
“Ninapendekeza
serikali ichangie nusu kwa nusu na mkulima ili kuvutia
uwekaji akiba katika
nchi na kuwa na sera ya uwekezaji katika maeneo
yatakayomwinua mkulima
kama miundombinu ya umwagiliaji, mikopo nafuu kwa
wakulima kwenye
pembejeo na nyumba na bima ya afya.
“Nimezungumzia umuhimu
wa uwazi katika matumizi ya fedha za umma ikiwemo
malipo ya watumishi na
viongozi wa umma. Nimewaeleza wananchi wa Nzega
kuwa siku ya Jumanne
kamati yangu ya Hesebu za Serikali (PAC) itaanza
kukagua mahesabu ya
vyama vya siasa nchini,” alisema.
Zitto alisema vyama
vya siasa vinatumia fedha za umma takribani sh
bilioni 20 kila mwaka
kama ruzuku, kwamba ni haki ya wananchi kujua
fedha zinatumika namna
gani.
Alisema kuwa wananchi
wa Nzega wana changamoto nyingi sana. Kwamba
wakulima wa pamba
walipewa madawa feki ya kuua wadudu, michango ya hovyo
hovyo ni mingi mno na
unyanyasi wa wana-CHADEMA ni mkubwa vijijini.
