Oct 8, 2013

MAANDAMANO YA KUMTAKA RAISI WA KENYA KUJIUZURU YAANZA KUANDALIWA, NI KUHUSU SAKATA LA AL SHABAAB




 

RAIS wa Kenya, Uhuru Kenyatta na Makamu wake, William Ruto, *sasa
wanakabiliwa na shinikizo la kutakiwa kujiuzulu, kutokana na shambulio
la kigaidi kwenye maduka ya Westgate.*   Hatua hiyo imekuja baada ya kuwako kwa habari kwamba viongozi hao wa juu
pamoja na serikali kwa ujumla walikuwa na taarifa za kutokea kwa
shambulio hilo kabla halijatekelezwa Septemba 21, mwaka huu. Tayari taasisi na watu wa kada mbalimbali nchini Kenya wamewataka
viongozi hao kuwajibika kutokana na kile walichodai kuwa walishindwa
kuchukua hatua kuzuia tukio hilo, licha ya taarifa za kutosha walizokuwa
nazo Shinikizo hilo limekuja baada ya ripoti ya kiintelijensia yenye jumla la
maneno 8,800 kunaswa na vyombo vya habari nchini Kenya, ikielezea
taarifa zote za kutokea kwa tukio la kigaidi kati ya Septemba 13 na 21. *Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Rais Kenyatta, Makamu wake Ruto, Mkurugenzi
wa Idara ya Usalama wa Taifa (NIS) Brigedia Michael Gichangi, Waziri wa
Mambo ya Ndani Joseph Lenku, wote walikuwa na taarifa za kutokea kwa
shambulio hilo.* Ni taarifa hizo ndizo ambazo zimeushtua umma wa Kenya, ambapo hivi
karibuni taasisi zisizo za kiserikali, ikiwamo ile inayoongozwa na Okiya
Omutata *zimetishia kuwaongoza Wakenya kuingia mtaani kuwaondoa
madarakani Rais Kenyatta na Makamu wake endapo hawatawajibika wao wenyewe.* Mbali na hilo, *taarifa za sasa za Al-Shabaab kudai kuwa walizungumza na
Rais Uhuru Kenyatta na kumpa onyo la kufanya shambulizi la kigaidi
nchini mwake ndizo zilizoamsha hasira za Wakenya wengi*, kwamba kiongozi
huyo anaujua ukweli halisi kuhusu tukio hilo. Kupitia akaunti yao ya twitter, ambayo ilifungwa baada ya shambulio la
Westgate, lakini ilifunguliwa tena hivi karibuni, Al-Shabaab walidai
kuwa katika mazungumzo yao hayo na Rais Kenyatta, walimuonya juu ya
uwezekano wa kufanya shambulio la kigaidi Westgate au kwenye Bunge la
nchi hiyo. Katika ujumbe wao huo wa kwenye twitter, Al-shabab walichapisha
mazungumzo baina yao na yule waliyedai Rais Uhuru Kenyatta.  Wiki iliyopita, gazeti la Standard lilikariri ripoti ya siri ya
Intelijensia yenye namba 184/2012 iliyowasilishwa Septemba 21, 2012,
ambayo ilikuwa ikieleza juu ya kuwako kwa mipango ya siri ya magaidi
kutekeleza shambulio katika ardhi ya Kenya.    Ripoti hiyo ilieleza juu ya kuwako kwa watu watatu wanaodhaniwa kuwa ni
magaidi, waliokuwa wametua Nairobi wakipanga shambulio la kujitoa mhanga
katika tarehe ambazo hazikujulikana. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, washirika wa Al Shabaab, wako Nairobi wakiwa
na mpango wa kutekeleza shambulizi la kujitoa mhanga, wakilenga Westgate
Mall na Holy Family Basilica. Ripoti hiyo iliwataja Sheikh Abdiwelli Mohamed, Sheikh Hussein na Sheikh
Hassan kuwa wanaaminiwa kumiliki ‘Vest’ mbili za kujitoa mhanga, mabomu
12 ya kurushwa kwa mkono na bunduki mbili aina ya Ak 47 na kwamba tayari
walikuwa wameandaa maeneo ya kutekeleza mashambulizi.  “Magaidi wamekuwa chini ya usaidizi wa Sheikh Hassan, maarufu kwa jina
la Blackie wa Majengo na Omar Ali, maarufu kwa jina la Jerry, ambao
wanaishi karibu na kituo cha mafuta cha Mamba na Huruma Mosque,
pembezoni mwa barabara ya Juja,” Gazeti hilo lilikariri sehemu ya ripoti
hiyo ya NIS. Pia ripoti hiyo ya NIS ilionesha kwamba watu wawili wanaosadikiwa ni
magaidi wenye asili ya Kisomali kutoka kikundi cha Al Shabab waliingia
Sudan Kusini kwa kupitia Djibouti, Eritrea na Sudan, kisha Uganda, kabla
ya kutumia mpaka wa Busia au Malaba kuingia nchini Kenya. Kwa mujibu wa gazeti hilo la Standard, ripoti hiyo ilieleza kwamba,
magaidi hao walisaidiwa na Teskalem Teklemaryan, ambaye ni mwandishi
anayeishi nchini Uganda na Sudan Kusini.   Kwamba wawili hao walikuwa wamebeba bunduki moja ya kivita aina ya GPMG,
mabomu manne ya machozi, mkanda mmoja wa risasi, bunduki tano aina ya AK
47, vazi la kuzuia risasi ambalo namba yake haijulikani na ramani
mbalimbali za mji wa Nairobi. Ripoti hiyo ilifafanua kwamba, Maalim Khalid, maarufu kwa jina la Maalim
Kenya, ambaye anahusishwa na matukio ya milipuko mbalimbali ya mabomu,
anatambulika kama mkuu wa mipango ya kigaidi nchini Kenya. Maalim Khalid alielezewa katika ripoti hiyo ya NIS kwamba alihusika na
shambulizi la kigaidi katika kituo cha Mchakos, Jengo la Assanands na
Bellavista Club mjini Mombasa. Pia ripoti hiyo inamhusisha Maalim Khalid na mpango wa kuteua vijana 20
wa Kenya ambao aliwapeleka katika miji ya Mark na Barawe, kwa ajili ya
kupewa mafunzo ya kigaidi. Kuvuja kwa taarifa hizo kulikuja ikiwa ni siku chache tangu kutekelezwa
kwa shambulio la kigaidi lilioua watu zaidi ya 67 katika maduka ya Westgate. Kamati ya Bunge inayohusika na masuala ya usalama, ilikwishamuweka
kitimoto Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa wa Kenya (NIS), Jenerali Michael
Gichangi, ili aeleze kama kuna uzembe wa kiusalama uliosababisha magaidi
hao kutimiza azima yao. Wabunge wa nchi hiyo wanaamini kwamba kulikuwa na upungufu ndani ya
Idara ya Upelelezi ya Usalama wa Taifa, hali ambayo iliruhusu magaidi
kupanga na kutekeleza shambulizi la Westgate Mall.