Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) Mh. Abdul Mombokaleo, Oktoba 16, 2025 amezindua rasmi KISSAN COMPANY LIMITED, katika mahafali ya 57 ya kidato cha nne katika shule ya Sekondari Kibaha.
Kuzinduliwa kwa kampuni hiyo inayoundwa na baadhi ya wahitimu wa zamani wa shule ya Sekondari Kibaha (Kibaha Alumni), kunalenga kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuchangia maendeleo ya nchi, hasa eneo la kuboresha elimu na mazingira ya kusomea nchini.
Awali kabla ya kuanzishwa kwa KISSAN, Alumni hao, tarehe 24/04/2025, wakiambatana na aliyekuwa mgeni rasmi katika mahafali ya kidato cha sita ambaye pia ni Alumni wa Kibaha Sekondari, Mh. Mombokaleo, waliipatia shule hiyo Kompyuta 20 na vifaa vyake na kuwezesha upatikanaji wa mtandao (internet) kwa mwaka mzima.
Kwa mujibu wa Alumni hao, wazo la kuanzishwa kwa kampuni hiyo lilizaliwa mara tu baada ya mahafali ya kidato cha sita na kwamba pamoja na mambo mengine, Kampuni hiyo inalenga kushiriki kuboresha mazingira ya elimu katika shule waliyosoma na Shirika la Elimu Kibaha kwa ujumla.
Katika mahafali hayo ya kidato cha nne, 2025, Mh. Abdul Mombokaleo na Alumni wenzake kupitia KISSAN na wadau wengine , wameipatia shule hiyo vifaa vya kisasa vilivyofungwa katika maabara mpya ya Kompyuta pamoja na vifaa vya kuzalisha umeme kwa kutumia nishati ya jua.
Vifaa vilivyotolewa katika ufadhili huo ni kompyuta 31 na vifaa vyake, viti 31, meza 16, printer 1, projector 1, projector screen 1, white board 1, server 1, solar panel 30 kila moja ikiwa na watt 585.
Naye Mkuu wa shule ya Sekondari Kibaha, Bw. George Mariot Kazi amesema, kwa sasa wameanza rasmi kutumia mfumo wa umeme kwa kutumia nishati ya jua kwenye maabara zao za kompyuta na madarasa janja pamoja na madarasa mengine yaliyo karibu na maabara hizo na hivyo kufanya ufundishaji uwe endelevu bila kuathiriwa na changamoto ya kukatika kwa Umeme.







