May 11, 2017

Nimemuomba Zuma atausaidie mkopo - Magufuli

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini Mhe. Jacob Zuma wakiwa wamesimama huku Nyimbo za Mataifa mawili zikiimbwa Ikulu jijini Dar es salaam Mei 11, 2017.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amesema amemuomba Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini Mhe. Jacob Zuma amuombee mkopo katika Umoja wa nchi tajiri BRICS ambapo Afrika Kusini nao wapo katika umoja huo.  
Rais Magufuli amesema hayo leo Ikulu wakati wakisaini mikataba ya ushirikiano kati ya Tanzania na Afrika Kusini ambapo wamekubaliana kushirikiana katika nyanja mbalimbali ikiwepo ushirikiano wa kiuchumi, utalii, na sekta ya sayansi na teknolojia.
"Nimemshukuru Rais Jacob Zuma kwa ujumbe wake na kuongozana na wafanyabiashara kutoka Afrika ya Kusini, ambao saizi wanakutana na wafanyabiashara wa kwetu jambo ambalo litaweza kuongeza uhusino wa kibiashara, tumekubaliana kuendelea kushirikiana ili kukuza fursa kati yetu, tumekubaliana nchi zetu kuondoa vikwazo vya kiuchumi ili tuweze kupiga hatua zaidi. Lakini pia nimemuomba Rais Zuma kutusaidia kupata mkopo wa bei nafuu katika umoja wao wa (BRICS) nchi tajiri ili usaidie ujenzi wa Reli ya standard gauge na amenihakikishia atafanya hivyo" alisema Rais Magufuli 
Mbali na hilo Rais Magufuli alimuomba Rais Zuma kuja kuchukua walimu wa Kiswahili nchini ili wakafundishe Kiswahili huko Afrika Kusini na kuzisi kuimarisha umoja wao, kwa upande wake Rais Jacob Zuma alishukuru mwaliko wa Rais Magufuli na kusema amefurahia sana huku akiahidi kuendeleza umoja na undugu huo kwa kutekeleza yale ambayo wamekubaliana.