Rais Dk. John Magufuli.
VIJANA watano wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kumdhalilisha
Rais Dk. John Magufuli na Jeshi la Polisi kutokana na mauaji ya askari
polisi wanne waliouawa na majambazi katika eneo la Mbande na Vikindu,
Dar es Salaam hivi karibuni.
Washtakiwa hao walifikishwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu, Dar es Salaam mbele ya mahakimu watano tofauti na kusomewa
mashtaka na Wakili wa Serikali, Salum Mohammed.
Walisomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Emmilius Mchauru,
Huruma Shahidi, Margareth Bankika, Dk. Yohana Yongolo na Respicius
Mwijage.
Akisomewa mashtaka, mshtakiwa Dennis Mtegwa anadaiwa Agosti 24,
mwaka huu eneo la Ubungo External kupitia mtandao wa WhatsApp, aliweka
maoni katika group linaloitwa Dsm 11 4u Movement, akisema‘JPM sijui
anawaza nini kichwani… hata samahani hajui au nilikosea hajui’, ‘nchi
imefika hapa kwa sababu ya mtu mmoja aliyeamua kujilipua ufahamu wake’,
‘sijaona tatizo kwa hilo, ila kwa huyu bwana misimamo ambaye amesema
msinijaribu na ilhali kajaribiwa na ubwabwa wa jubilee kusema yote’.
‘Siasa si chuki wala upinzani si uadui, ajifunze kushindana kwa
hoja sio mitutu ya bunduki na mazoezi yasiyo na kichwa wala miguu ya
polisi’.
Mshtakiwa Suleiman Saidi anadaiwa Agosti 25, mwaka huu maeneo ya Kigogo, kwa kutumia mtandao wa Facebook, aliandika ‘Safi sana aisee, mi naona wangekufa kama 20 hivi halafu Simon Sirro tumuulize mazoezi wanafanyia wake zao au’.
Katika kesi nyingine, mshtakiwa Juma Mtatuu akiwa eneo la Ocean
Road, Agosti 24, mwaka huu anadaiwa kuwa alituma ujumbe katika Facebook
akisema ‘Huyu hata akifa ataenda peponi, na kufanya mazoezi kote kule
wamekufa Mbagala, mimi nitakuwa wa kwanza kuandamana kule Kahama,
tarehe moja naelekea Kahama kwa Ukuta, mimi nitakuwa namba moja kushika
bendera ya Ukuta, kifo kipo tuu, usiogope kwani mawe na mapanga
yameisha’