
Wachimbaji Wadogo Wadogo
Serikali
kupitia Wizara ya Nishati na Madini imepanga kuwapatia ruzuku
wachimbaji wadogo wa madini ili kuongeza mchango wa madini katika pato
la taifa kutoka asilimia 3.5 ya sasa hadi 10.
Hayo
yamesemwa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo
wakati wa mahojiano ya kipindi maalum cha Tunatekeleza kinachorushwa na
kituo cha Televisheni ya Taifa(TBC).
“Sekta
ya Madini inachangia asilimia 3.5 ya pato la Taifa,lakini dhamira yetu
ni kwamba wakati tunaingia kuwa nchi ya kipato cha kati madini yanapaswa
kuchangia si chini ya asilimia kumi”
Aidha
aliongeza kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi
ya viwanda ifikapo 2025, hivyo adhma ya Wizara yake ni kuongeza kasi ya
pato linalotokana na sekta ya madini na
Aliongeza
kuwa ili mafanikio hayo yafikiwe Serikali imekusudia kupandisha hadhi
ya wachimbaji wadogo ili wafikie ngazi ya kuwa wachimbaji wa kati na
hivyo sekta hii itachangia pato la Taifa kwa kiasi kikubwa.
Aidha
Waziri Muhongo alisema kuwa Serikali imepokea pesa mkopo wa Tsh. Bilioni
3 kutoka Benki ya Dunia na imepanga kutoa ruzuku ya vifaa kwa
wachimbaji hao wakati wowote kuanzia sasa.
“Serikali imeshaanza kutoa maeneo na kufikia tarehe 15 septemba tutaanza kutoa ruzuku kwa wachimbaji hao” alisema Prof. Muhongo.
Akizungumzia
hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kuzuia utoroshaji wa madini
nje ya nchi Profesa Muhongo alisema kuwa tangu mwaka 2012 Wizara yake
iliweka madawati ya ukaguzi wa madini katika viwanja vya ndege vya
Mwalimu Nyerere Jijini Dar es Salaam,Kilimanjaro na Mwanza na
wakafanikiwa kukamata madini zaidi ya tani kumi.