Mamlaka
ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali itakuwa na uwezo na mamlaka ya
kuchunguza watu waliozaliwa na jinsi mbili na kubaini jinsi tawala yenye
nguvu zaidi. Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa
Serikali wa Mwaka 2016, uliopitishwa juzi usiku saa nne bungeni unampa
Mkemia Mkuu mamlaka ya kuchunguza na kubaini jinsi ya mtu na kutatua
utata kwa mtu atakayekuwa amezaliwa na jinsi mbili.
“Waheshimiwa wabunge naona wengi wenu
mnadhani mkemia mkuu kazi yake ni kuchunguza vinasaba kubaini uhalali wa
mzazi na mtoto, maana naona wabunge wengi wamelishabikia hilo, lakini
katika teknolojia ya vinasaba yanahusu pia utambuzi wa jinsi, watu
unakuta wanawake au wanaume wanazaliwa jinsi ya kike na kiume, kwa hiyo
tunaangalia jinsi tawala ni ipi ina nguvu,” alisema Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.
Bi. Ummy alikuwa akijibu michango ya
wabunge waliochangia wakati wa kujadili Muswada wa Mamlaka ya Maabara ya
Mkemia Mkuu 2016 kabla ya kuupitisha juzi usiku, waliotaka mamlaka ya
maabara ya mkemia mkuu kutoa elimu kwa wananchi juu ya shughuli zake.
Alisema kwa sheria hiyo, sasa mkemia
mkuu kupitia maabara yake anaweza kusema jinsi ya kike au ya kiume ndio
yenye nguvu, lakini pia kuna suala la kuhakikisha utambuzi wa mwanadamu
hasa wakati yanapotokea majanga pamoja na watu wanaosafiri kwa makundi.
Alikubaliana na wabunge kuwa iko haja ya
kuwaelimisha wananchi juu ya kazi za maabara ya mkemia mkuu ambao wengi
wao wanadhani inafanya kazi hiyo tu ya kubaini vinasaba vya mzazi na
mtoto, lakini sasa wafahamu hata waliozaliwa na jinsi mbili wanaweza
kutegua utata huo kwa kubaini jinsi tawala au jinsi yenye nguvu zaidi
kama ni ya kiume au ya kike.
Alisema Maabara ya Mkemia Mkuu wa
Serikali imekuwepo kihistoria tangu mwaka 1890 na imekuwa chombo cha
kiserikali cha uchunguzi cha kikemia wa kimaabara kwa bidhaa mbalimbali
na kuongeza kuwa imekuwa ikifanya uchunguzi wa kikemia wa vyakula, dawa
na vipodozi hasa pale inapotokea utata au kuhusisha masuala ya kesi za
jinai.