
September 19, 2016 Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA jimbo
la Temeke kimemfukuza uanachama Diwani na Mwenyekiti wake kutoka kata ya
Kurasini, Matiti Claudian Togocho kutokana na kashfa ya ufisadi wa
zaidi ya shilingi milioni 400 alizozipata kwa njia ya udanganyifu.
Taarifa iliyotolewa na Benard Mwakyembe ambaye ni Mwenyekiti wa
Chadema wilaya ya Temeke imeeleza kuwa mnamo November 23 2015, Diwani
huyo akiwa na wenzake wanadaiwa walitengeneza hati feki ya nyumba tano
za James Makundi aliyekuwa mpangaji kwenye nyumba zake kisha kufanya
hujuma ya kuvunja nyumba hizo kwa amri ya uongo ilitolewa na wakili
kishoka wa Samora Avenue badala ya amri ya mahakama ikiwa ni kwa lengo
la kujipatia pesa kutoka kwa mwekezaji ambazo ni zaidi ya shilingi
milioni 200.
Diwani huyu pia anahusishwa na matukio mengine mawili ya udhulumaji
wa zaidi ya shilingi milioni 140 za mirathi ya marehemu Peter Christian
Kijeni wakati kesi ikiwa mahakamani pamoja na fedha za fidia za Paulina
Shaban na wajukuu zake ambao Diwani huyo alisimamia nyumba zao
kubomolewa.
“Kutokana na maamuzi ya chama baada ya kujiridhisha na makosa
yake na kwa mujibu wa katiba ya chama chetu, mamlaka za mwisho zimefikia
maamuzi ya kumvua uanachama wake hivyo atakuwa amepoteza sifa za kuwa
Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Mivinjeni pamoja na nafasi yake ya
Udiwani kata ya Kurasini.” Alisema Benard Mwakyembe