
Ujenzi wa Daraja
la Salender litakalounganisha eneo la Coco Beach na eneo Agha Khan kupitia
baharini Jijini Dar es Salaam unatarajiwa kuanza Mwezi Juni Mwakani baada ya
Serikali ya Tanzania kukamilisha mchakato wa upatikanaji wa fedha za ujenzi kutoka
benki ya Exim ya Korea.
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amesema hayo leo tarehe 22
Septemba, 2016 muda mfupi baada ya kufanya Mazungumzo na Balozi wa Jamhuri ya
Korea hapa nchini Mhe. Song Geum-Young, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Rais Magufuli
amesema ujenzi wa daraja hilo litakalokuwa na urefu wa kilometa 7 zikiwemo
kilometa 1.4 zitakazopita baharini, unatarajiwa kukamilika mwaka 2020 na daraja
hilo litasaidia kupunguza adha ya msongamano wa magari katika Jiji la Dar es
Salaam.
"Mchakato wa
kulijenga hili daraja la Salender unaendelea vizuri kwa sababu hivi sasa
kampuni ya Kikorea ambayo inafanya usanifu ipo kwenye hatua za mwisho na zabuni
zinategemewa kutangazwa mwezi wa tatu Mwaka kesho na zitakwenda haraka, kwa
hiyo mambo yakienda vizuri ujenzi unaweza kuanza mwezi wa sita, bahati nzuri
fedha zote zipo na zimeshatolewa na Benki ya Exim ya Korea"
Amesema Rais Magufuli.
Aidha, Dkt.
Magufuli amemshukuru Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete
kwa juhudi alizozifanya zilizowezesha kujengwa kwa hospitali ya Mloganzila kwa ufadhili wa Jamhuri ya Korea na kwamba
hospitali hiyo itakuwa ya kisasa zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Amesema ujenzi wa
Hospitali hiyo unatarajiwa kukamilika kabla ya mwisho wa mwaka huu na kwamba
tayari Madaktari na Wataalamu takribani 100 waliopata mafunzo nchini Korea na
wenye ujuzi wa namna ya kutumia teknolojia inayowekwa kwenye hospitali hiyo
wapo hapa nchini.
Rais Magufuli
ambaye ameelezea nia ya Serikali ya Tanzania kufungua ofisi za Ubalozi Mjini
Seoul nchini Korea ameongeza kuwa Serikali yake imedhamiria kuendeleza na
kuimarisha uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya nchi hizi kwa lengo la
kuwaletea manufaa wananchi ikiwemo kutumia teknolojia na ujuzi wa nchi ya Korea
katika ujenzi wa Meli.
Kwa upande wake,
Balozi wa Korea hapa nchini Mhe. Song Geum-Young ametoa salamu za pole kufuatia
maafa ya tetemeko la Ardhi yaliyotokea Mkoani Kagera na mikoa jirani, na
ameahidi kuwa Korea itatuma timu ya wataalamu kuja kuona namna ya kusaidia.
Balozi Song
Geum-Young pia amemhakikishia Rais Magufuli kuwa Korea itaendeleza na
kuimarisha uhusiano wake na Tanzania na kwamba itatoa ushirikiano wa kutosha
kufanikisha miradi ya maendeleo ambayo inatekelezwa hapa nchini ikiwemo ujenzi
wa Daraja la Salender, Meli, Hospitali ya Mloganzila na mingineyo.
Wakati
huo huo, Rais Magufuli amekutana na kufanya Mazungumzo
na Balozi wa Urusi hapa nchini Mhe. Yuri Popov ambapo viongozi hao wamekubaliana
kuendelea kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa kihistoria baina ya nchi hizo
huku wakitilia mkazo katika kukuza biashara na uwekezaji.
Pamoja na hayo Balozi
Yuri Popov amepongeza na kuelezea kufurahishwa na hatua zinazochukuliwa na Rais
Magufuli katika kuimarisha uchumi huku akibainisha kuwa kwa hatua hizi anaamini
ajenda ya kujenga uchumi wa viwanda itafanikiwa.
Katika
hatua nyingine, Rais Magufuli amepokea taarifa ya
hali ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali na katika mazungumzo yake na Mkemia
Mkuu wa Serikali Prof. Samwel Manyele, amemtaka kuendelea kuimarisha utendaji
kazi wa maabara hiyo ili kuongeza ufanisi wa majukumu yake ambayo ni kufanyia
uchunguzi vielelezo vya makosa ya Jinai na usimamizi wa sheria za udhibiti wa
kemikali na udhibiti wa vinasaba vya binadamu (DNA).
Gerson
Msigwa
Mkurugenzi
wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es
Salaam
22
Septemba, 2016