Mkurugenzi
wa Sheria, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Ibrahim
Ngabo, akizungumza na waandishi wa Habari wakati Mkuu wa Mkoa wa Tanga
alipotembelea eneo la Chongoleani itakapojengwa gati itakayotumika
kupakua mafuta ghafi.
Mkuu
wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigella, akiongea jambo mara baada ya
kutembelea eneo la Chongoleani Mkoani Tanga, itakapojengwa Gati
itakayotumika kupakua mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda.

Mkuu
wa Mkoa wa Tanga , Martine Shigella ( Wa tano kutoka kulia), katika
picha ya pamoja na Wawakilishi kutoka Wizara ya Nishati na Madini,
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Mamlaka ya Bandari
Tanga . Pia yupo Meya wa Jiji la Tanga na Mkurugenzi wa Jiji la Tanga.

Maandalizi
ya awali ya kuandaa eneo itakapojengwa Gati itakayotumika kupakua
mafuta ghafi ya kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga
yakiendelea.
Picha kwa Hisani ya www.tangaraha.tz.blogspot.com
Na Asteria Muhozya, Tanga.
Mkuu
wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigella amesema, tayari Mkoa huo umeanza
maandalizi ya awali ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Bomba la Mafuta
Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), kutoka Hoima nchini Uganda hadi
Bandari ya Tanga.
Shigella
aliyasema hayo mwanzoni mwa juma alipotembelea eneo la Chongoleani
Tanga itakapojegwa gati ya kushusha mafuta ili kuona maandalizi
yanavyoendelea na kuongeza kuwa, Mkoa huo unaandaa mazingira ya
kutekeleza mradi husika ambapo tayari barabara ya kuelea eneo hilo
imekwishachongwa.
“Tunajenga
mazingira ya kutekeleza mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi, lakini pia
tunao wajibu wa kuboresha Bandari yetu kwa ajili ya utekelezaji huo.
Yale tunayoweza kufanya sisi kama Serikali tayari tunaanza wakati
tukisubiri Marais na Mawaziri wa nchi husika kusema ni lini ujenzi huu
utaanza rasmi. Kwetu ni fursa na tunataka maendeleo.”
Kwa
upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Bandari ya Tanga, Henry Arika alisema
kuwa, katika maandalizi ya mradi huo, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari
(TPA) imetenga jumla ya Shilingi bilioni 9.2 kwa ajili ya kuboresha
miundombinu ya bandari hiyo ili kuwezesha mapokezi ya vifaa vya mradi
husika.
Aliongeza
kuwa, mbali na kuboresha miundombinu, fedha hizo pia zitatumika
kuongeza kina cha gati ili kuwezesha Meli kubwa zitakazobeba vifaa vya
ujenzi kuweza kutia nanga kwa urahisi.
“TPA
inatarajia kupokea wastani wa tani 250,000 za shehena za vifaa kupitia
Bandari yetu wakati wa maandalizi na ujenzi wa bomba hilo, hivyo
maboresho kwetu ni muhimu sana. Tunajua kazi kubwa iliyo mbele yetu,
tunajipanga na tunajiandaa kuhakikisha kwamba mizigo inapita kwa ufanisi
na usalama,” alisema Arika.
Alifafanua
kuwa, ili kuimarisha usalama na kupanua wigo wa eneo la kuhifadhi
mizigo, tayari Mamlaka hiyo imetenga eneo la ukubwa wa kilomita za mraba
2,600 litakalotumika kwa shughuli za kuhifadhia shehena ya mizigo kabla
ya kusafirishwa, ikiwemo pia maandalizi ya ujenzi wa mashine maalum ya
ukaguzi (scanner) kwa ajili ya kukagulia mizigo ili kuimarisha usalama.
Naye,
Mkurugenzi wa Sheria kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania
(TPDC), Ibrahim Ngabo alisema kuwa, majadiliano ya mfumo wa Kisheria
kuhusu mradi kati ya nchi za Tanzania na Uganda yamekwishaanza na
yanaendelea vizuri.
Kwa
upande wake, Kaimu Kamishna wa Nishati anayeshughulikia masuala ya
Petroli, Wizara ya Nishati na Madini, Mwanamani Kidaya, alisema kuwa,
amefurahishwa na namna Mkoa huo ulivyoanza maandalizi ya utekelezaji wa
mradi husika na hivyo kuwataka wananchi kuwa tayari kuupokea mradi huo
ikiwemo kutumia fursa zitakazojitokeza kupitia mradi husika.
Katika
ziara ya kutembelea eneo hilo, Mkuu wa Mkoa alifuatana na Uongozi wa
Mkoa akiwemo Meya na Mkurugenzi wa Jiji hilo, Uwakilishi kutoka Wizara
ya Nishati na Madini, TPDC na TPA.