Mkurugenzi
wa Idara ya Habari MAELEZO,Hassan Abbasi akifafanua mikakati yake
mbalimbali kuhusiana na Idara hiyo,kwenye mkutano wake wa kwanza wa
kujitambulisha na pia kuzungumza na Waandishi wa habari katika ukumbi wa
Idara hiyo mapema leo asubuhi jijini Dar,Mkurugenzi huyo kwa mara ya
kwanza leo amekutana na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali
tangu kuteuliwa kwake hivi karibu.
Mkurugenzi
wa Idara ya Habari MAELEZO,Hassan Abbasi akijibu maswali mbalimbali
yaliyokuwa yakiulizwa kuhusiana na mikakati yake ambayo aliitaja,kulia
ni Mkurugenzi Msaidizi, Vicent Tinganya.

MKAKATI WA KUWAELEZA WANANCHI UTEKELEZAJI WA AHADI ZA SERIKALI
Dar es Salaam, Ijumaa, Agosti 19, 2016:
Serikali
kupitia Idara ya Habari-MAELEZO itaanza kutekeleza mikakati mbalimbali
inayolenga kuwapatia wananchi taarifa za kila mara kuhusu utekelezaji wa
ahadi zake. Mikakati hiyo itakayosaidia kuongeza uwazi na ushirikishaji, pamoja na mambo mengine, itahusisha hatua zifuatazo:-
Mosi,
kuboresha mfumo wa mawaziri na watendaji waandamizi Serikalini
kuzungumza na wananchi ili kuainisha utekelezaji wa vipaumbele vya
bajeti, sera na mipango ya Taifa. Kuanzia Agosti 25 mwaka huu, mawaziri
wataanza kuzungumza na umma kupitia vyombo vya habari kueleza vipaumbele
vya bajeti zao na utekelezaji wake hadi kufikia sasa.
Pili,
kuanzisha utaratibu wa Idara ya Habari-MAELEZO kueleza kwa umma kila
mara, na haraka iwezekanavyo, utekelezaji wa sekta zote katika ngazi ya
kitaifa. Msemaji Mkuu wa Serikali atakuwa akitoa taarifa hizo kuanzia
hivi karibuni.
Tatu,
Serikali itaimarisha ushirikiano zaidi na wadau mbalimbali katika
kutekeleza mikakati yake ya mawasiliano kwa umma. Pamoja na wadau
wengine, Serikali itahakikisha inafanyakazi kwa karibu na vyombo vya
habari ili vishiriki vyema katika ujenzi wa Taifa.
Mwisho,
wakati huu Idara ikiendelea kufanyiakazi mikakati mingine ili kuboresha
mawasiliano kwa umma, naomba wadau wote kutoa ushirikiano kwangu
binafsi, Idara niliyopewa kuiongoza hivi karibuni na zaidi tumuunge
mkono Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli katika ajenda yake ya mageuzi
kupitia HapaKaziTu.
Imetolewa na:
Hassan Abbasi,
Mkurugenzi Idara ya Habari-MAELEZO.