
Mkuu wa Wilaya ya
Kinondoni, Mh Ally Hapi leo ametengua uteuzi wa aliyekuwa Kaimu Mganga
Mkuu Mfawidhi wa Hospitali ya Mwananyamala Dkt. Delila Mushi kwa kosa la
kupandisha bei ya baadhi ya huduma kinyume cha taratibu na sheria.
Mushi amedaiwa
kupandisha bei ya huduma hizo baada ya kukaa kikao cha hospitali pasipo
kuipeleka hoja ya kupandisha bei katika kikao cha Idara ya Manispaa na
huduma za jamii.
Taratibu alizotakiwa
kufuata Mushi ni kuipeleka hoja hiyo Manispaa, ambapo ingejadiliwa
kwenye kikao cha huduma za jamii kisha baraza la madiwani kuipitia na
kuitolea maamuzi jambo ambalo hakulifanya badala yake alipandisha bei
pasipo kupitia taratibu hizo.
Bei ya huduma
zilizopandishwa ni pamoja na bei ya kadi ambapo wagonjwa waliofika
katika hospitali hiyo bila ya barua ya rufaa kutoka vituo vya afya na
zahanati zilizo karibu nao, walitakiwa kulipa sh 10,000 badala ya 6,000.
“Hakuna jambo baya kama
kiongozi kufanya maamuzi pasipo kufuata utaratibu halafu maamuzi hayo
yakaathiri wananchi wanyonge, mkurugenzi nakuagiza hiyo bei ya kadi
irudi kama ilivyokuwa awali, huwezi mlipisha mgonjwa kiasi kikubwa cha
fedha huku huduma unazotoa haziendani na bei hiyo, ” amesema Hapi.
“Hakuna sababu ya
anayekaimu nafasi ya mganga mkuu kwa sasa kubaki na wadhifa huo wakati
haumtoshi, atatafutwa mwIngine kuja kuwa mganga Mkuu, ”amesema.
Kwa sasa ameteuliwa Dkt. Daniel Nkungu kukaimu kwa muda wadhifa huo hadi atakapoteuliwa mganga mwingine kushika wadhifa huo.
Hata hivyo, Baada ya
Hapi kutoa agizo la kutenguliwa uteuzi wa Dkt. Mushi na kuamuru Wagonjwa
kulipa bei ya kadi ya awali, baadhi ya wahudumu wa mapokezi waligoma
kutoa huduma kwa madai kuwa mifumo ya utoaji risiti imeharibika.
Mariam Hamisi Sahabani mkazi wa Kinondoni, alifafanua jinsi wahudumu hao walivyogoma baada ya mkuu wa wilaya kuondoka.
“Baada ya Mheshimiwa
kuondoka wamegoma kutoa huduma kwa kigezo kuwa mashine ilikuwa mbovu,
inawezekanaje? Mbona wakati tunalipa 10,000 mashine zilifanya kazi,
iweje sasa zisifanye? ” alihoji.
Kufuatia malalamiko hayo
yaliyotolewa na wananchi waliokuwepo kwenye hospitali hiyo, Mganga mkuu
wa Manispaa ya Kinondoni Dkt. Aziz Msuya alisema atawasimamisha kazi
waliogoma kutoa huduma kwa kuwa walikuwa na lengo la kupinga kauli ya
serikali.
“Naagiza huduma ianze kutolewa kuanzia sasa, na watakaogoma kutoa huduma nitawasimamisha kazi kuanzia kesho, ”amesema Msuya.