CHAMA cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema) Kanda ya Dar es Salaam, kimemkaribisha Kamanda wa
Polisi wa Kanda hiyo, Kamishna Simon Sirro kujitokeza na kuwa mstari wa
mbele kwenye maandamano ya Operesheni Ukuta yatakayofanyika Septemba
Mosi.
Kimesema kinamkaribisha kamanda huyo ili kuondoa uwezekano wa kupelekewa taarifa za uongo na askari wake kuhusu maandamano hayo.
Makamu Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya
Dar es Salaam, Benard Mwakyembe, alisema jana kuwa hakuna haja ya
kamanda huyo kukaa ofisini bali ajitokeze katika Operesheni Ukuta na awe
mstari wa mbele kuwapiga wananchi ambao watatumia muda huo kumuuliza
maswala ya sheria kuhusu maandamano hayo.
“Lengo la Operesheni Ukuta ni kuwaeleza wananchi kuwa nchi yetu haifuati sheria bali inafuata mawazo ya mtu mmoja.
“Tumwambie tu kwamba Kamanda Sirro
ngoma hii ya Ukuta si ya kitoto, vitisho na mbwembwe zake anazozionyesha
barabarani hazitutishi, tupo tayari kwa lolote.
“Tumejiandaa kisaikolojia kwa namna
yoyote, tupo tayari kufa kwa ajili ya kuwatetea wananchi, na Meya wa
Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita, atakuwa mstari wa mbele pamoja na
viongozi wengine,” alisema Mwakyembe.
Aidha alisema maandalizi yote yamekamilika kwa asilimia 99.5 katika mitaa 582 na kata 102 ya jiji zima la Dar es Salaam.
“Niwashukuru Umoja wa Vijana wa
Chama Cha Mapinduzi (UV-CCM) kwa kutuunga mkono kuandaa maandamano yao,
tunaamini haya ya kwetu yamewapa motisha na kuamua kufanya ya kwao.
“Ninaliomba Jeshi la Polisi liwape
ulinzi wa kutosha ingawaje sisi tunajua kwamba huo ni mtego walioufanya
kisiasa ili kuleta mabishano ambayo hayana nafasi kwetu,” alisema.
Alisema haki za vyama vya siasa ni
kutoa maoni ya kisiasa kadiri vitakavyoona inafaa, ili kutekeleza sera
zake kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa na Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Katiba ya Zanzibar.