Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
makazi, William Lukuvi akisalimiana na Mpima ardhi mkuu wa kanda ya kaskazini Nina Rutakyamirwa, alipofika wilayani Kiteto
kuzindua Baraza la Ardhi na Nyumba la wilaya hiyo (kushoto) ni mkuu wa Mkoa
huo, Dk Joel Bendera.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
makazi, William Lukuvi akisalimiana na Kaimu Msajili msaidizi wa baraza la
ardhi na nyumba wa kanda ya kaskazini Zena Happe alipofika wilayani Kiteto
kuzindua Baraza la Ardhi na Nyumba la wilaya hiyo (kushoto) ni mkuu wa Mkoa
huo, Dk Joel Bendera.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
makazi, William Lukuvi akimtambulisha kwa wananchi Mwenyekiti wa Baraza la
ardhi na nyumba la Wilaya ya Kiteto Charles Mnzava, alipozindua baraza hilo.
WANANCHI wa Wilaya ya Kiteto Mkoani
Manyara waliokuwa wanasafiri kwa kilometa 320 kwenda Wilayani Simanjiro na
kurudi kufuata huduma ya Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya, hvi sasa wamemaliziwa
kero hiyo baada ya Wziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya makazi, William
Lukuvi kuzindua Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Kiteto.
Waziri
Lukuvi akizungumza wakati akizindua baraza hilo alisema, kero ya wananchi
wa wilaya ya Kiteto kufuata huduma hiyo umbali wa kilometa 320 kwenda na kurudi
wilayani Simanjiro ambapo kuna baraza kama hilo, ili kufungua mashauri yao
kwenye masuala ya ardhi au nyumba limemalizika.
“Baraza hilo litawasaidia wananchi wa
Kiteto kuondoa kero ya kufuata huduma hiyo wilayani Simanjiro kwani kati ya
kesi 150 zinazofanyika kwa mwaka wilayani Simanjiro, kesi 100 zinawahusu watu
wa wilaya ya Kiteto,” alisema Lukuvi.
Alisema mpango wa matumizi bora ya ardhi
utasababisha wakulima na wafugaji kutogombana kwani kila kijiji kitatenga eneo
la mashamba, malisho ya mifugo, makazi, sehemu za ibada na huduma nyingine na
kuondokana na migogoro.
Kwa upande wake, mkuu wa mkoa wa
Manyara, Dk Joel Bendera alisema baraza hilo litasaidia kumaliza tatizo la
migogoro ya ardhi iliyokithiri kwani awali wananchi wengi walikuwa wanafika
mjini Babati kutoa malalamiko yao ya migogoro ya ardhi.
Dk Bendera aliwataka Mwenyekiti wa
baraza hilo la Kiteto Charles Mnzava na wazee wa baraza kutenda haki kwa
wananchi wa Kiteto wakati wa kuendesha mashauri hayo ili jamii ione faida ya
kuwepo kwa baraza hilo.
Hata hivyo, Mbunge wa jimbo la Kiteto,
Emmanuel Papian alimshukuru Waziri Lukuvi kwa kuzindua baraza hilo kwani
litasaidia kwa namna moja au nyingine kumaliza migogoro ya ardhi ambayo ilikuwa
imekithiri kwenye eneo hilo la Kiteto.
Papian alisema kupitia baraza la ardhi
na nyumba hapa Kiteto huo ndiyo utakuwa mwisho wa kuwepo kwa migogoro ya ardhi
kwani awali walikuwa wanateseka kwenda Simanjiro kwani jamii ilikuwa inatumia
gharama kubwa.