
Mkuu
wa Kampuni ya Zantel Zanzibar Mohammed Mussa Baucha akizungumza wakati
wa hafla ya kukabidhi vifaa kwa ajili ya Kambi ya wagonjwa wa
kipindupindu iliyofanyika Wizara ya Afya Mnazimmoja (kushoto) Waziri wa
Afya Mahmoud Thabit Kombo (kulia) daktari dhamana kanda ya Unguja Dkt.
Fadhil Mohammed.

Mkuu
wa Kampuni ya Zantel Zanzibar Mohammed Mussa Baucha akimkabidhi Waziri
wa Afya baadhi ya vifaa vilivyotolewa na Kampuni hiyo kwa ajili ya Kmbi
ya wagonjwa wa kipindupindu (kushoto) Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt.
Juma Malik Akili.

Shehena ya msaada wa vifaa vilivyotolewa na Kampuni ya Zantel kwa ajili ya kambi ya kipindupindu Zanzibar.

Waziri
wa Afya Mahmoud Thabit Kombo akitoa shukrani baada ya kupokea msaada
huo wenye thamani ya shilingi milioni kumi na moja. Picha na Makame
Mshenga-Maelezo Zanzibar.
Kampuni ya simu ya mikononi ya Zantel leo imetoa msaada wa vifaa
vya usafi kwa ajili ya kusaidia juhudi za kupambana na kipindupindu za Serikali
ya mapinduzi ya Zanzibar kwa ajili ya kambi za kipindupindu visiwani humo.
Vifaa hivyo ambavyo vimekabidhiwa kwa Wizara ya Afya vimegharimu
jumla ya shlingi milioni 11, ni pamoja na matanki ya kuhifadhia maji, vitanda
vya kamba, pampu ya kisima, mabomba ya kunyunyizia dawa, maturubali mazito,
maboksi ya gloves na mafuta ya petroli lita 3,000 kwa ajili ya magari ya
kuhudumia kambi za kipindupindu.
Akizungumza wakati wa kupokea vifaa hivyo, Waziri wa Afya,
Mheshimiwa Mahmoud Thabit Kombo amesema ugonjwa wa kipindupindu ambao mpaka
sasa umesabababisha vifo vya watu 53 utatoweka visiwani Zanzibar baada ya wiki
tatu zijazo.
‘Kwa kiasi kikubwa juhudi zetu za kupambana na kipindupindu kwa
kushirikiana na mamlaka mbalimbali zimeanza kufanikiwa, na tunaomba wadau
wengine wazidi kujitokeza kutuunga mkono’ alisema Mahmoud.
Akikabidhi msaada huo kwa niaba ya kampuni ya Zantel, Mkuu wa
kampuni ya Zantel upande wa Zanzibar, Mohammed Mussa amesema kampuni yake
inajivunia kushirikiana na serikali ya Zanzibar kupambana na ugonjwa wa kipindupindu
ambapo ameeleza kuwa tarehe 23 na 24 mwezi uliopita kampuni ya Zantel imetuma
ujumbe kwa wateja wake zaidi ya laki sita na nusu juu ya kujikinga na ugonjwa
huo.