
Na Mwene Said wa Blogu ya Jamii, Dar es Salaam.
SHIRIKA
la Umeme Tanzania (Tanesco) limesema kukatikatika kwa umeme linapata
hasara ya Sh. Milioni 500 kwa siku na kwamba watanzania waelewe ni
matatizo ya kiufundi halina lengo la kuwakomoa wananchi.
Akizungumza
na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Mkurugenzi Mtendaji
wa Tanesco, Felichesmi Mramba alisema hali ya kukatika umeme
inayoendelea nchini ni kutokana na marekebisho ya baadhi ya mitambo ya
kuzalisha umeme na mifumo ya gesi inayomilikiwa na kampuni binafsi
inakwamisha upatikanaji huduma hiyo kwa uhakika.
Alisema
suala hilo halihusiani na siasa bali ni matatizo ya kitaalamu ambayo
hata shirika linapata hasara na wakati mgumu kwa kushindwa kuwapatia
huduma sahihi wateja wao.
“Baada
ya bomba la gesi kukamilika, visima viwili kati ya vine vilianza
kuingiza gesi kwenye bomba Agosti 22, mwaka huu kule Mtwara na ilifika
jijini Dar es Salaam, Septemba 5, mwaka huu … hata hivyo gesi hiyo
ilifika ikiwa na msukumo wa bars 2 na kwamba ilichukua wiki mbili
kufikia bars 37 kuwezesha kuwasha mitambo ya megewati 90” alisema na
kuongeza kuwa.
“Mtambo
wa Kinyerezi kazi inaendelea hadi wataalamu watakaporidhika kwamba
mabomba yote ni masafi na yanaweza kuanza kuwashwa tayari kwa kutoa
huduma… kukamilika kwa mitambo hiyo kutatuhakikishia jumal ya megawatio
305 zaidi ya umeme unaopatikana sasa”alisema Mkurugenzi Mramba.
Akifafanua
zaidi alisema mbali na umeme wa gesi hali ya mabwawa yanayozalisha
umeme kwa sasa hayana maji ya kutosha baadhi yanaelekea kukauka.
Alitaja
mabwawa hayo na kiwango chake cha maji kuwa, Mtera Uwezo wake wa juu ni
megawati 800, uzalishaji wake wa sasa ni sifuri (0), Kidatu 204 kwa
sasa 27, Kihansi, 180 kwa sasa 51.5 New Pangani Falls, 68 kwa sasa 17,
Hale 21 kwa sasa 4 na Nyumba ya Mungu ni 8 kwa sasa 5.5.
Alisema
shirika linasikitishwa na taarifa za uzushi zinazotolewa kwenye
mitandao ya kijamii kwamba mitambo ya Kinyerezi ni chakavu haiwezi
kufanyakazi kwamba siyo kweli zina nia ya kulichafua shirika hilo.