Jaji mstaafu Damian Lubuva akizungumza
na viongozi wa Chadema. Kutoka kulia ni Wakili wa chama hicho, John
Malya na Reginald Munisi.
Mkurugenzi wa NEC, Ramadhani Kailima, ndiye aliyetoa ufafanuzi huo
wakati akizungumza na Nipashe jana kuhusiana na mashine hizo ambazo
zilikamatwa juzi wakati zikiendelea kutumiwa kwa shughuli ya
uandikishaji wa wafanyakazi wa kiwanda hicho kilichopo katika eneo la
Mikocheni.
Wakati Polisi wakizikamata jana kwa ushirikiano na maofisa kadhaa
wa NEC, tayari mashine hizo zinavyofanana na BVR zilishaandikisha
wafanyakazi zaidi ya 100 wa Kiwanda cha MM Steel.
Akielezea zaidi kuhusiana na tukio hilo, Kailima alisema kuwa, mara
baada ya kupata taarifa za kuwapo kwa mashine hizo, walienda kuzikagua
na kubaini kuwa hazina uhusiano na zile za Biometric Voter Registation
(BVR), zilizotumiwa na wao (NEC) kuandikisha wapiga kura kwa ajili ya
Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 25.
“Hakuna ukweli wowote kuwa zile ni mashine za BVR na tumebaini ni
feki, tena ni sawa na zile zinazotumika kwenye ofisi mbalimbali
kuandikisha wafanyakazi wake... hawa waliosema ni mashine za
kuandikishia wapiga kura hawako sahihi... si kweli,” alisema Kailima.
Alisema endapo watu wataendelea kuwa na shaka juu ya namna NEC
inavyofanya kazi kwa sababu tu ya kuona mashine kama hizo, basi wanaweza
pia kukamata mashine za ofisi nyingi zikiwamo za kwenye viwanja vya
ndege, hospitali na hata manispaa kama ya Kinondoni ambayo hutumia
mashine kama hizo kwa shughuli zake mbalimbali.
“Mashine tulizozikuta kwenye hiyo ofisi jana (juzi) ni computer
mpakato (laptop) na mashine za kuchukua alama za vidole. Hata wale
wafanyakazi tulipowahoji walibainisha kuwa wanazitumia kuorodhesha
wafanyakazi wao kwa ajili ya usalama wa ofisi... na tena zipo ofisi
nyingi zinatumia mashine hizo,” alisema Kailima.
Kailima alitoa tahadhari kwa wataalamu wanaovishauri vyama vya
siasa kuwa makini na kuacha kupotosha kwa kuwaleza mambo yasiyo na
ukweli, hasa kuhusiana na NEC kwani wao wanafanya kazi zao kisayansi
zaidi na hakuna fursa ya kuwapo kwa ubabaishaji wa aina yoyote.
Aliongeza kuwa hawafanyi kazi zao kwa misikumo ya kisiasa, bali
huzingatia utaalamu na hivyo wanaotumiwa kwa ushauri na vyama waache
kuwadanganya wanasiasa.
“Hawa wanasiasa wanadanganywa na watu wanaojiita wataalamu... mashine hizi (zilizokamatwa) hazihusiani na BVR," alisisitiza.
CHADEMA WAHUSISHWA UCHUNGUZI
Akieleza zaidi juu ya hatua walizochukua baada ya tukio la juzi,
Kailima alisema kuwa (jana) walifanya uchunguzi wa mashine hizo kwa
kushirikiana na wawakilishi kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) ambao ndiyo walitoa malalamiko kwao kuhusiana na madai ya
kuwapo kwa mashine kama BVR zinazotumiwa kuandikisha watu.
“Wataalamu wao (Chadema) walikuja na tukathibitisha (wote) zile ni
feki na hazihusiani kabisa na mashine zetu za BVR,” alisema Kailima.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema) John Mnyika, aliitaka NEC ivikabidhi vyama vya siasa
nakala za daftari la kudumu la wapiga kura ili kuepukana na njama za
wizi wa kura alizodai zinaweza kufanywa na chama tawala -- Chama Cha
Mapinduzi (CCM).
Akizungumia tukio la juzi kuhusu kukamatwa kwa vifaa vinavyofanana
na mashine za BVR, Mnyika alisema suala hilo walilikabidhi kwa maofisa
wa NEC na Jeshi la Polisi ambao wanalichunguza kwa kushirikiana na
maofisa wa Chadema ili kubaini ukweli.
Kadhalika, Mnyika aliitaka NEC kushughulikia suala hilo haraka na
kutishia kuwa wasipotoa majibu ya kina ndani ya siku tatu, atashauri
wanachama wenzake kuishinikiza ifanye hivyo ili kuondoa shaka iliyopo.
Hata hivyo, Mnyika aliyasema hayo kabla ya kutolewa kwa maelezo ya
Kailima kuhusiana na uchunguzi walioufanya kwa mashine hizo
zilizokamatwa Mikocheni.
Juzi, Chadema walipata taarifa kutoka vyanzo vyao vyao kuwa kuna
mashine zinazofanana na BVR zinaandikisha watu na hivyo wakashirikiana
na Polisi na NEC kuvikamata kabla ya kwenda kuvichunguza. Meneja
Mawasiliano wa MM Steel, Aboubakar Mlawa, alieleza kuwa kampuni yao
imeamua kuandikisha wafanyakazi wao kwa nia ya kudhibiti usalama vitendo
vya wizi, na kwamba tayari walishaandikisha wafanyakazi zaidi ya 100
kati ya 900 waliokuwa wakitarajiwa kutoka kwenye viwanda vyao saba.
CHANZO: NIPASHE