MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chadema kupitia mwamvuli wa Ukawa, Edward Lowassa, anatarajia kuhudhuria mazishi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrati (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, imefahamika.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrati (DP), Mchungaji Christopher Mtikila enzi za uhai wake.
Duru za siasa kutoka ndani ya Ukawa, zimebainisha kwamba, licha ya
kusambazwa kwenye mitandao kwa taarifa za Mchungaji Mtikila kumshambulia
Lowassa kwa maneno kabla ya kifo chake, lakini mgombea huyo wa Ukawa
amepanga kwenda kuhudhuria mazishi hayo kutokana na sababu kadhaa.“Kwanza amesema Mtikila ni miongoni mwa waasisi wa siasa za mageuzi nchini na ametoa mchango mkubwa katika mambo mbalimbali yaliyobadilisha demokrasia na kupanua wigo wa siasa za upinzani,” kilisema chanzo chetu kutoka ndani ya Ukawa.
Lakini pili, kwa mujibu wa chanzo hicho, ni kushindwa kuhudhuria misiba kadhaa ya wanasiasa waliofariki dunia katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.
Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema kupitia mwamvuli wa Ukawa, Edward Lowassa.
Mchungaji Mtikila alifariki kwa ajali ya gari Jumapili, Oktoba 4, 2015 katika Kijiji cha Msolwa mkoani Pwani wakati akirejea Dar es Salaam kutoka Njombe alikokwenda kufanya mkutano wa hadhara. Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Mazishi ya mwanasiasa huyo, David Mwaijojele, mwili wa marehemu utasafirishwa leo kwenda Ludewa, Njombe na endapo kila kitu kitakwenda sawa, Mchungaji Mtikila atapumzishwa kaburini kesho.