Ronaldo akibusu kiatu cha dhahadu alichokabidhiwa kama tuzo.
SALEH ALLY
MSHAMBULIAJI nyota duniani, Cristiano
Ronaldo, amefikisha mabao 500 aliyoyafunga akiwa na timu tatu pamoja na
timu yake ya taifa.
Ronaldo amefikisha mabao 500 katika
kipindi ambacho ametimiza miaka 30, jambo ambalo si dogo au si la
kuliacha lipite tu. Hakika Ronaldo ambaye amekuwa mwanasoka bora duniani
mara tatu, ana kipaji cha juu kabisa. Mabao hayo na mfano utaona
amefikisha mabao 323 sawa na gwiji wa Real Madrid, Raul Gonzalez si
jambo dogo. Sasa ana nafasi ya kuwa gwiji kwa kufunga mabao mengi zaidi.
Tayari Ronaldo ana rekodi ya wastani wa
juu zaidi katika ufungaji kwenye Ligi Kuu Hispania ‘La Liga’. Ana
wastani wa 1.05 ya mabao. Maana yake amefunga bao katika kila mechi kama
mabao yake yatagawanywa.
Mafanikio ya mabao 500 tangu alipofunga
bao lake la kwanza akiichezea Sporting Lisbon ya Ureno Oktoba 7, 2002.
Ndani ya miaka 13, Ronaldo ameweza kufunga mabao hayo 500 tena akicheza
katika timu kubwa tatu ambazo hakika zinakuwa na ushindani wa juu na
wachezaji wake hupambana na upinzani wa juu kabisa. Ameshinda kila kombe
kwa ngazi ya klabu akiwa na Manchester United na Real Madrid ambazo ni
moja ya timu kubwa tatu zaidi duniani.
Wakati anatua Real Madrid, msimu wa
kwanza aliweza kuweka wastani wa mabao 20 kwa msimu. Baada ya hapo
akapanda kwenda hadi mabao 53, kitu ambacho si mzaha hata kidogo. Msimu
wake wa kwanza naalifunga mabao 21, uliofuata wa 2010/11 akatandika
kimiani mabao 50. Msimu wa 2011/12, akafunga mabao 66, msimu wa 2012/13
akashuka kwa kufunga mabao 51, ule wa 2013/14 akafunga mabao 56 na
2014/15 akafunga mabao 66.
Angalia ushindani wa La Liga au michuano
ya Ulaya, lakini huyu mtu ana uwezo wa kufunga hadi mabao 50 kwa zaidi
ya misimu miwili au mitatu
anafanya hivyo. Katika hali ya kawaida
unaamini kweli ni kipaji pekee? Ndiyo maana nikaamua kukumbusha kwamba
mafanikio ya watu hawa hayapatikani ukiwa umelala na kufumba macho.
Lazima kujituma, lazima kujipambanua na
kuamini mtafutaji hachoki. Historia ya Ronaldo inajielezea, kwa kuwa
wazazi wake walikuwa ni watu wa maisha ya chini kabisa.
Baba yake alikuwa ni mtunza bustani tu
huko kwao katika Kisiwa cha Madeira, Ureno. Ronaldo alionyesha anataka
kufanikiwa na utaona wakati akiwa Manchester United wachezaji wengi
walimshangaa kwamba anaishi vipi, kweli anaweza kula raha na maisha
yake. Kwamba hakuwa akijipa nafasi ya kula maisha? Maana alikuwa akifika
mazoezini saa moja au mbili kabla ya wenzake, aliondoka mazoezini saa
moja baada ya wenzake. Muda wote aliokuwa pale aliendelea kujifua zaidi.
Hata walipokwenda gym, yeye ndiye alibaki muda mwingi zaidi ya wengine.
Kuna wakati hadi Kocha Sir Alex Ferguson aliwahi kumuonya kufanya
hivyo, kwamba apunguze mazoezi.
Wakati anatokea Manchester United kwenda
Madrid, wengi walichambua na kusema angefunikwa kabisa na Lionel Messi
na kupotea. Lakini leo amebaki pekee anayechuana vikali na mshambuliaji
huyo wa Barcelona mwenye kipaji cha juu kabisa. Ronaldo si mashine, ni
binadamu kama wewe lakini ameamua kuishi tofauti, ameamua kutaka
kufanikiwa. Amepania kutimiza ndoto zake bila ya kusikiliza maneno mengi
ya pembeni ambayo hukatisha tamaa.
Hii inakuhusu wewe mchezaji wa soka wa
Tanzania katika daraja lolote, achana na woga na kusikilizasana maneno
ya watu hasa yale yanayosisitiza ‘hauwezi’. Unaweza zaidi ya
wanavyofikiri, unaweza kufika zaidi ya ulipo. Lakini usifumbe macho
ukalala. Hauwezi kuwa kama Ronaldo, lakini unaweza kupata mafanikio ya
juu yanayoweza kuwashangaza wengi kama Mreno huyo anavyoshangaza kwa
mabao yake hayo 500.
Kwa Tanzania hata kufunga mabao 50 kwa
misimu minne nayo ni shida kubwa. Bado wewe unaweza kuwa wa kwanza kama
utaachana na woga, kukubali kukatishwa tamaa. Ronaldo si mashine, ni
binadamu lakini anafanikiwa. Lakini lazima ukubali kuumia zaidi na
kujituma zaidi ili kufikia mafanikio. Usiyaache mafanikio yake ya mabao
500 yapite tu kama kitu cha kukushangaza, badala yake yafanyie kazi siku
nyingine yakusaidie hata katika maisha ya kawaida. Panga ndoto, iote
ukipambana na mwisho ufanikiwe.
BAO LA KWANZA AKIWA….
SPORTING LISBON
Oktoba 7, 2002 vs Real Betis.
MAN UNITED
Novemba Mosi, 2003 vs Portsmouth.
REAL MADRID
Agosti 29, 2009 vs Deportivo.
TIMU YA TAIFA URENO
Juni 12, 2004 vs Ugiriki.
MABAO:
NDANI YA BOKSI: 417
NJE YA BOKSI: 83
PENALTI: 81
ADHABU: 45
ALIFUNGAJE?
Mguu wa Kulia: 326
Mguu wa kushoto: 89
Kichwa: 83
TIMU ALIZOZIFUNGA LA LIGA:
Sevila-21, Getafe-18, Barcelona-15,
Atletico Madrid-15, Malaga-14
WALIOMPA ‘ASISTI’ NYINGI:
Karim Benzema 31, Mesut Ozil 28,
Angel di Maria 20, Gareth Bale 15,
Ryan Giggs 16, Gonzalo Higuain 15.