Makundi kumi kati ya makundi 15
yaliyoshiriki katika kinyang’anyiro cha kuingia katika nusu fainali ya
mashindano yanayokuwa kwa kasi hapa nchini ya Dance 100% yanayoandaliwa
na kituo cha televisheni cha East Africa(EATV) chini ya udhamini wa
kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania,yanaendelea ambapo mwishoni
mwa wiki tulishuhudia hatua ya robo fainali kufanyika katika uwanja wa
Don Bosco Oysterbay jijini Dar es Salaam na kushirikisha makundi 15
kutoka wilaya 3 za mkoa wa Dar es Salaam.
Makundi yaliyofanikiwa kuingia nusu fainali
ni Wazawa Crew,Majokeri,Quality boys,The best,The best boys kaka
zao,Team Makorokocho,The winners, The W.D, Cute babies na Team ya
shamba.Mratibu wa mashindano hayo,Happy Shame,alisema kuwa katika
kinyang’anyiro cha robo fainali hiyo walipata makundi 10 hayo ambayo
yameingia moja kwa moja katika ngazi ya nusu fainali.
“Huu ni mwaka wa nne East Africa
Televisheni tunaandaa mashindano haya chini ya udhamini wa Vodacom
Tanzania na mwaka hadi mwaka mashindano haya yamekuwa yakiongezeka
kupata umaarufu na kuwavutia vijana wengi kila kona ya nchi yetu ambao
wamekuwa wakijitokeza kushiriki”Alisema Shame.
Shame, aliongeza kwamba kundi litakaloibuka
na ushindi katika mashindano haya ambayo pia yamekuwa yakionyeshwa na
kituo cha televisheni cha East Afrika kila jumatano saa moja kamili
usiku,litajishindia kitita cha shilingi milioni 5.
Naye Meneja Uhusiano wa Vodacom Tanzania
ambao ni wadhamini wakuu wa mashindano haya,Matina Nkurlu alisema kuwa
Vodacom inatoa udhamini kwa kutambua kuwa muziki na michezo ni maeneo
ambao yanaweza kutoa ajira kwa vijana na kuweza kuwakwamua kimaisha.
Alisema kuwa Vodacom inatambua kuwa jukumu
la kukabiliana na tatizo la ajira hapa nchini sio la serikali peke yake
bali pia ni la watu wote ikiwemo makampuni,taasisi za umma na za binafsi
na ndio maana siku zote imekuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono
jitihada za kupambana na tatizo la ajira kupitia nyanja mbalimbali
ikiwemo michezo , burudani na huduma mbalimbali zinazotolewa na kampuni
hiyo.
“Vodacom tunaamini kuwa vijana wanaweza
kuleta mapinduzi makubwa katika sekta mbalimbali iwapo
watawezeshwa,hivyo tunadhamini mashindano haya tukiamini kuwa vijana
wenye vipaji wanaoshiriki wataweza kujitangaza na kujulikana ambapo
katika siku za usoni ni rahisi kujiajiri kupitia katika sanaa”Anasema
Nkurlu.
Aliwataka vijana waamke hususani wasichana
wasibaki nyuma na watumie fursa kama hizi ili waweze kujikomboa kiuchumi
“Suala la ajira sio kufanya kazi ofisini tu bali kuna njia nyingi za
kujiajiri na kujipatia mapato mojawapo ikiwa ni kupitia michezo,muziki
na sanaa nyingine na Vodacom siku zote tutakuwa mstari wa mbele kuunga
mkono jitihada za vijana kujikwamua kiuchumi”Alisisitiza Nkurlu.