Dar es Salaam. Kiongozi wa ACT –
Wazalendo, Zitto Kabwe (pichani) amesema kuwa chama chake
hakitashirikiana na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa), badala yake kitasimama chenyewe kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba
25.
Kauli hiyo inazima minong’ono iliyotawala miongoni
mwa wanachama wa ACT-Wazalendo waliokuwa wakimuuliza Zitto kuhusu chama
hicho kujiunga na Ukawa.
Zitto alimaliza uvumi huo jana
jijini hapa katika mkutano na viongozi wa chama, wanachama na watiania
wa nafasi mbalimbali katika Uchaguzi Mkuu.
Alisema
ACT-Wazalendo haiwezi kuungana na Ukawa inayoundwa na vyama vya Chadema,
CUF, NCCR-Mageuzi na NLD kwa vile sera ya chama hicho tofauti na vyama
hivyo.
“Nawaomba niwatoe hofu, Chama cha ACT-Wazalendo
kitasimama chenyewe kama kilivyo, hatutaki ushirikiano,” alisema Kabwe
na kuongeza:
“Najua chama chetu bado ni kichanga, kina
miezi mitano tangu kuanzishwa kwake, lakini si mnajua Timu ya Soka ya
Mbeya City?” aliwauliza wajumbe waliojibu: “ndiyo.”
“Ile
timu ilianza kama masihara, lakini mwisho wa siku ikawa tishio kwa timu
za Ligi Kuu, basi chama hiki kitakuwa hivyo,” alisema Zitto na
kushangiliwa na wajumbe waliohudhuria mkutano huo.”
Alibainisha kuwa chama chake kimedhamiria kuwatumikia Watanzania na kushika dola kwa njia halali.
Alisema
ACT – Wazalendo kina azimio la Tabora, ambalo ndani yake kuna kipengele
namba nne, kinachozungumzia miiko na mali za viongozi kabla ya kujiunga
na chama hicho na kwamba chama chochote kitakachotaka kujiunga ACT,
lazima kikubaliane na kipengele hicho ili kuzuia mianya ya rushwa na
uroho wa madaraka ndani ya chama.
Aliwataka wanachama kutotishika na mtikisiko wa kisiasa utakaotokea muda wowote kuanzia wiki hii, kwani ni mambo ya kawaida.
“Mtikisiko
huu usiwatie presha, mtulie tena mnyooshe miguu juu, huu ni upepo wa
kisiasa na wala haututoi kwenye mstari. Narudia tena viongozi wangu ACT,
mkoa msiyumbishwe na hali itakayojitokeza,” alisema.
“Hatuna presha kufanya vikao vya mara kwa mara, chama kwa masilahi ya watu fulani, tutafuata ratiba yetu vizuri,” alisema Zitto.
Alisema ACT-Wazalendo kinaendeshwa na wanachama na siyo viongozi, hivyo kila uamuzi hufuata kanuni na taratibu za chama.
“Ndiyo
maana kuna chama kimoja (hakukitaja), hadi leo (jana) kinapiga danadana
kumtangaza mgombea wake wa urais sijui wanamsubiri atoke kwenye Sayari
ya Mars,” alihoji Zitto.
Zitto alisema kuwa
atashirikiana na wagombea wote watakaopitishwa na chama hicho kugombea
nafasi mbalimbali ili majimbo 10 ya Mkoa wa Dar es Salaam yaende
ACT-Wazalendo.
“Juzi nilikuwa Jimbo la Kigoma Mjini,
kuna chama kimoja kilikuwa kinatafuta mgombea atakayewakilisha jimbo
hilo maana kila anayeambiwa anakataa, kwa sababu wanasema ni ngome ya
ACT-Wazalendo,” alisema.
chanzo: MWANANCHI
