Geita. Mamia ya wakazi wa
Wilaya ya Sengerema na Mkoa wa Geita jana walijitokeza katika mapokezi
ya mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk John Magufuli yaliyopambwa na
mbio za wapiga kasia katika Ziwa Victoria.
Dk Magufuli
akitokea Mwanza, alivuka Ziwa Victoria na kuingia Sengerema huku wavuvi
waliokuwa wakitumia mitumbwi wakipeperusha bendera za CCM na kukizunguka
kivuko cha Mv Misungwi alichokuwa ameabiri pamoja na msafara wake.
Msafara
wa Dk Magufuli ulioanzia kwenye Kivuko cha Busisi saa 3.35 asubuhi
ulisimamishwa mara kadhaa na wananchi ambao walikuwa wamefunga barabara
wakiwa na matawi ya miti na wengine wakitembea kuusindikiza.
Dk
Magufuli ambaye alikuwa ameambatana na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa
CCM, Nape Nauye na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Tanzania Bara, Rajabu
Luhwavi alikuwa akisimama kwenye gari la wazi na kuwapungia wananchi
waliyokuwa wamejipanga kwenye Barabara Kuu ya Geita- Bukoba.
Mapokezi
ya Dk Magufuli yaliongozwa na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja
ambaye gari lake ndilo lililokuwa limetangulia huku likisimama kwenye
makundi ya watu na kuwapanga kutokana na wingi wao. Msafara huo pia
uliongozwa na ving’ora vya polisi, huku ukiwa umetawaliwa na magari ya
wabunge wa CCM kutoka mikoa mbalimbali ya Kanda ya Ziwa.
Geita yarindima
Msafara
wa Dk Magufuli ulifika mkoani Geita saa 5.30 asubuhi na barabara
zilifungwa kwa dakika 15 wakati mgombea huyo akisalimiana na wakazi wa
mkoa huo.
Akizungumza wakati akisalimiana na wakazi wa
Sengerema na Geita, Dk Magufuli alisema amepita kuwasalimu na huku
akiwaahidi kuwa hatawaangusha...
“Nimekuja kuwasalimia,
itoshe kusema kwamba sitawaangusha. Nimefundisha shule ya Sekondari
Sengerema hivyo hapa ni nyumbani,” alisema Dk Magufuli.
Awali,
Dk Magufuli alianza kwa kuimba wimbo wa Kisukuma, “aliselema” huku
wananchi wakiitikia ‘alija’ “aliselema”, ‘alija’ “selema, selema, aleja,
ng’wana ngosha, ‘aleja.’ Wimbo huo unamaanisha “anasukuma, anakwenda,
mtoto wa kiume, anakwenda.”
Baada ya kuimba wimbo huo,
Dk Magufuli alianza kwa kuwashukuru wananchi wa Geita kwa mapokezi
makubwa ambayo hayajawahi kutokea tangu awe kiongozi... “Wana Geita
nawashukuruni sana kwa mapokezi haya... yanaonyesha ni mapokezi ya
ushindi, nimebaki na deni kubwa kwenu, nitawatumikia wananchi wote na
sitawaangusha, sitajali chama nitawatumikia wote wa CUF, UDP, Chadema,
CCM sitajali huyu ni wa chama gani, nashukuru sana wananchi wa Geita,”
alisema na kuongeza: “Leo si siku ya kampeni, nikianza watasema nimeanza
kampeni mapema. Mimi napenda kusema kwamba wanashukuru sana wana Geita
kwa sala zenu zilizonifikisha hapa leo, nitafanya kazi kwa ajili ya
Watanzania wote, sitawabagua.”
