Dodoma. Historia inaelekea kujirudia, kama
ilivyokuwa wakati Rais Jakaya Kikwete akizindua Bunge la 10 na wabunge
wa Chadema kususia hotuba yake, ndivyo itakavyokuwa atakapolihutubia
Bunge kwa mara ya mwisho Alhamisi bila kuwapo wabunge hao na wenzao
kutoka NCCR – Mageuzi na CUF wanaounda Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
(KUB).
Wabunge wa Chadema wakati huo wakiunda KUB peke
yao, walisusia hotuba ya Rais Kikwete Novemba 30, 2010 wakipinga matokeo
ya uchaguzi uliomweka madarakani.
Safari hii wakati Rais Kikwete akitarajia
kulihutubia Bunge hilo kwa mara ya mwisho kabla ya kulivunja rasmi kwa
tangazo la Serikali (GN) litakalotolewa baadaye, hali inaelekea kuwa
vilevile, lakini kutokana na sababu tofauti.
Kiongozi wa KUB, Freeman Mbowe alisema jana kwamba
wabunge wanaounda kambi hiyo hawatahudhuria vikao vilivyosalia kwa
sababu ya Serikali kupitisha miswada mitatu ya petroli na gesi kinyume
cha kanuni na sheria.
“Miswada hii inahitaji umakini mkubwa kabla ya
kuigeuza kuwa sheria,” alisema Mbowe na kufafanua kuwa utaratibu
uliotumika utazaa sheria mbaya.
Alisema KUB na viongozi wote wa vyama vinavyounda
Ukawa walikubaliana kuishauri Serikali, uongozi wa Bunge na wabunge wa
CCM wasiwe na haraka katika kuipitisha miswada hiyo lakini
hawakusikilizwa.
Mbowe alisema walikubaliana kuiacha miswada hiyo
ipitishwe na Bunge la 11 litakaloanza Novemba ili kufanya uchambuzi wa
kina kwa kuzingatia masilahi mapana ya Taifa.
Alisema licha ya semina mbalimbali kati ya wabunge
wa pande mbili, kwa sababu wanazozijua wenyewe, Serikali na uongozi wa
Bunge waliamua kuendelea kuvunja kanuni za Bunge kwa kupitisha miswada
hiyo kwa utaratibu wa “voda fasta.”
“Tunatambua kuwa pamoja na maudhui mengine katika
miswada hii, kuna kipengele muhimu ambacho kinalazimisha mikataba yote
iliyosainiwa awali, ya gesi na mafuta, isibatilishwe.
“Mikataba ambayo leo hii ipo katika utekelezaji
imekuwa ikilalamikiwa na watu wengi kuwa ina mapungufu makubwa na hivyo
inalikosesha Taifa mapato mengi,” alisema Mbowe katika mkutano
uliohudhuriwa pia na baadhi ya wabunge wa CUF na Chadema.
Alisema kwa sababu uongozi wa Bunge
umewadhalilisha kwa kuwatoa wabunge 43 bungeni kinyume cha taratibu, ni
dhahiri ulikusudia kuipitisha miswada yote bila kujali ushauri.
Mbowe alisema uongozi unaomaliza muda wake una
agenda ya siri inayoufanya kulazimisha sheria hizo kupitishwa katika
utaratibu huo.
“Sisi wabunge wa Ukawa tumeshauriana na viongozi wengine wa
vyama vyetu, tumeona hatuna sababu ya kuendelea kuwapo ndani ya Bunge,
kushiriki katika kutunga sheria ambazo zitakuwa na athari kwa Taifa. Ni
kwa misingi hiyo, sisi wabunge wa Ukawa leo (jana) ndiyo mwisho katika
Bunge la Jamhuri ya Muungano.
Vyama kukutana leo
Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema alisema
chama hicho kimeitisha Kamati Kuu leo na vyama vingine vimeita vikao
kwenye vyama vyao kujadili suala hilo kabla ya kesho kufanya mkutano wa
wabunge wote wa Ukawa na viongozi wakuu wa vyama hivyo.
Alisema lengo la kikao hicho ni kupeana taarifa ya
nini kinaendelea ili azma yao ya kulipeleka suala hilo kwa wananchi
iweze kuwekewa utaratibu wa utekelezaji.
Kanuni zilizovunjwa
Waziri Kivuli na Katiba na Sheria, Tundu Lissu
alisema jambo la kwanza lililokiukwa katika kupitisha miswada hiyo ni
utaratibu wa kanuni za kuitangaza katika Gazeti la Serikali.
Alisema Kanuni ya 80 inasema kila mswada wa sheria
wa Serikali utatangazwa katika gazeti angalau katika matoleo mawili
kukiwa na muda usiopungua siku saba kati ya toleo la kwanza na la pili
lakini miswada hiyo ilitangazwa Mei 29 na mara ya pili Juni Mosi, ikiwa
ni tofauti ya siku tano tu.
Alisema pia kuwa mswada unatakiwa uwasilishwe,
ujadiliwe na kupitishwa kabla miswada mwingine, lakini kilichofanyika ni
kusoma yote na kuijadili kwa pamoja.
Alitaja pia Ibara ya 98 ya Katiba kuwa imekiukwa
kwa kuwa inataka mswada wa sheria unaohusu Muungano kuungwa mkono na
theluthi mbili ya kila upande, jambo ambalo halikutakiwa.
Lissu alisema wanapinga sehemu ya miswada hiyo
inayosema kuwa masuala yanayohusu fedha (mikataba) hayatabadilishwa na
Bunge kwa kipindi kisichopungua miaka mitano tangu kupitishwa kwa sheria
hiyo.
“Kifungu kingine tunachokipinga ni cha 261(3)
ambacho kinasema mikataba ya mafuta na gesi itaendelea kuwa halali chini
ya sheria hii hadi muda wa mikataba hii itakapoisha,” alisema.
Waziri Kivuli, Sera, Uratibu na Bunge, Rajab
Mbarouk Mohamed, alisema neno Zanzibar katika miswada hiyo limetajwa
mara moja tu na kuwa sehemu hiyo ya Muungano haijashirikishwa kwenye
kipengele cha ukusanyaji wa mapato yanayotokana na gesi na mafuta.
Ulinzi mkali bungeni
Jana, Polisi waliimarisha ulinzi bungeni kwa
kuongeza idadi ya askari na pia kufunga kipande cha barabara kuanzia
kwenye mzunguko wa kituo kikuu cha mabasi yaendayo mikoani kupitia eneo
la Bunge hadi mwanzo wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Tawi la
Dodoma.
Kulikuwa na idadi kubwa ya polisi wa usalama
barabarani, utepe mweupe uliofungwa katika barabara hiyo huku kukiwekwa
kibao kilichoandikwa kwa maandishi mekundu, “barabara hii imefungwa.”
Alipoulizwa kuhusu hatua hiyo, Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Dodoma, David Misime alisema kufungwa kwa barabara hiyo ni
miongoni mwa shughuli za usalamachanzo: mwananchi
