Ingawa hakuwa akitajwa mara kwa mara kwamba ni mmoja wa wagombea
tishio, kupitishwa kwa jina la Dk Asha-Rose Migiro kuingia katika tano
bora ya kuwania urais kwa tiketi ya CCM, siyo jambo la ajabu.
Rekodi yake kitaifa na kimataifa lakini pia
jinsia, ni mambo ambayo yamechangia kwa kiasi kikubwa Waziri huyo wa
Katiba na Sheria, kuvuka hatua hiyo ya kwanza.
Dk Migiro ambaye pia ni Katibu wa Halmashauri Kuu
ya Taifa, Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa ya CCM, alijitosa
katika safari ya kuelekea Ikulu Juni 15 pasi na mbwembwe za aina yoyote.
Mtanzania huyo ambaye aliweka rekodi ya kuwa
Mwafrika wa kwanza mwanamke kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa
(UN), alikuwa akitajwa kuwa anaweza kuwa mwanamke wa kwanza kuwa Rais wa
Jamhuri ya Muungano.
Hakuwahi kutangaza nia kama ilivyokuwa kwa makada
wengine waliotumia fursa hiyo kuelezea mikakati yao lakini pia, hakuwa
na mbwembwe katika kutimiza sharti la kusaka wadhamini mambo ambayo
pengine yalimwongezea sifa za kupitishwa miongoni mwa wagombea 38
waliokuwa wamechukua na kurejesha fomu kuomba nafasi hiyo ya juu kabisa
katika utawala wa nchi.
Lakini kigezo kingine kilichomvusha ni umakini
wake na kutokulengwa na mishale ya kashfa ambazo ziliwakumba mawaziri
kadhaa katika Serikali ya Awamu ya Tano na yote hayo yanampa fursa kubwa
ya kufika mbali katika safari yake hiyo hasa ikiwa hoja ya nafasi ya
wanawake kushika urais kama ilivyokuwa katika uchaguzi wa Spika wa Bunge
la 10 itatiliwa maanani.
Dk Migiro alianza kutajwatajwa miongoni mwa
wanaoweza kumrithi Rais Jakaya Kikwete baada ya kumaliza mkataba wake
Umoja wa Mataifa na kurejea nchini na mara moja kuteuliwa kuwa mbunge na
Waziri wa Katiba na Sheria.
Msimamo wake
Wakati akizunguka katika mikoa mbalimbali kusaka
saini za wadhamini, Dk Migiro alikuwa makini katika kuzungumza huku
akisisitiza kuwa anasubiri Ilani ya CCM... “Na mimi nitaweka mikakati ya
kuendeleza yale ambayo yameshafanyika. Sasa endapo nitapata ridhaa ya
chama changu, nyenzo yangu kuu itakuwa ni Ilani ya Uchaguzi ya CCM.”
Alisema kwa kuwa uchumi umeendelea kukua awamu
hadi awamu, naye atahakikisha kukua huko kunawafikia wananchi wengi
zaidi: “Nitahakikisha kuwa mambo haya yaliyofanywa na awamu za uongozi
zilizopita yanakuwa stahamilivu na endelevu na kuwafikia wananchi walio
wengi zaidi.”
Wasemavyo alikozaliwa
Gazeti hili limefanya mazungumzo na kaka yake,
Ally Shaban Mtengeti (79) ambaye anasema, Asha ni wa sita kuzaliwa
katika familia yao.
Anasema mdogo wake huyo hana makuu na anapenda watu lakini asiyependa kuonewa.
Mtengeti anasema Asha ana nyota ya uongozi kwa
kuwa alianza kuongoza tangu akiwa chuo kikuu ambako alikuwa mbunge
kwenye baraza la vyuo vikuu.
Wananchi wengi wa Tarafa ya Usangi wilayani
Mwanga, Kilimanjaro anakotokea, hawamfahamu kwa sura japo wamekuwa
wakimsikia kupitia vyombo vya habari.
Migiro anaishi zaidi nje ya Mwanga kwa sababu mama
yake ni mtu wa Dar es Salaam na kwa kiasi kikubwa amelelewa na mama na
Mwanga alifika baada ya kifo cha baba yake.
“Sijawahi kumuona lakini nimekuwa nikisikia jina
lake kwenye vyombo vya habari na hata huku anafika mara chache, lakini
kutokana na shughuli za hapa na pale sijawahi kufika kwake kumuona”
anasema Mohamed Kabewa, mkazi wa Kijiji cha Mshewa, Kata ya Chomvu.
Kauli ya Kabewa ya kutomfahamu kwa sura au
kutowahi kuzungumza na Dk Migiro ilizungumziwa na majirani zaidi ya
watano wanaozunguka nyumba ya Shaban Mtengeti ambaye ni baba mzazi wa Dk
Migiro.
Licha ya kutomfahamu, wananchi wa Chomvu na Tarafa
ya Usangi wanasema anazo sifa za kuongoza kwa kuwa amewahi kuwa
kiongozi katika maeneo mbalimbali na kote alikoongoza hajakumbana na
kashfa yoyote.
Kabewa anasema licha ya mfumo dume katika jamii, wananchi wanatakiwa kuangalia utendaji wa mtu na uwajibikaji wake.
Hata hivyo, wananchi wengine, Hussein Mkodo na
Rose Mfinanga wanaonyesha shaka kama mwanamke akipewa nafasi hiyo ya
ngazi ya juu nchini ataweza kuongoza kutokana na hali ya nchi ilivyo.
Wananchi hao walizungumzia kukithiri kwa vitendo
vya ufisadi na kuelezea shaka yao kama Dk Migiro ataweza kukemea hasa
ikizingatiwa kwamba hilo limewashinda viongozi wengi.
Mkodo anasema wenye fedha wanaonekana kuvinunua baadhi ya vyombo
vya dola na hivyo kuwa na nguvu kuliko vyombo hivyohivyo hali ambayo
anasema hata Dk Migiro akipewa nafasi hiyo ya uongozi wa juu, itamuwia
vigumu kupambana na wala rushwa.
“Dk Migiro ni msafi hatujasikia akituhumiwa popote lakini
Tuna shaka kama hao wanaosema Sh10milioni ni fedha
ya mboga, ataweza kuwashtaki maana watu hao wapo ndani ya chama,
”alihoji Mkodo.
Mkodo alisema kwa sasa Watanzania wanatakiwa
kufanya mabadiliko kwa sababu kwa miaka 50 wana kunywa pombe ileile,
wanachokifanya ni kubadili chupa tu.
Anasema Watanzania wanaishi kwa mashaka kwa kuwa
viongozi wameshindwa kusimamia masuala nyeti na kusababisha wananchi
kuishi ya taabu, huku wanasiasa wakijinufaisha kupitia mgongo wa
wanyonge.
chanzo: MWANANCHI
