Dodoma/Z’bar. Wakati vikao vya juu vya CCM vya
kuchuja wagombea urais vikianza leo, hofu na wasiwasi umezidi kutanda
miongoni mwa wagombea, viongozi na wanachama wa chama hicho kuhusu namna
ya kuikabili minyukano baina ya wagombea hao na kibarua cha Uchaguzi
Mkuu wa Oktoba.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa miongoni
mwa mambo yanayoleta hofu na kusababisha presha kuongezeka kila kukicha
ni woga wa kufanya makosa katika uteuzi wa ndani, hali inayoweza
kukigharimu chama hapo baadaye hasa kutokana na kuongezeka nguvu ya
upinzani.
Kutokana na hali hiyo kumekuwa na shinikizo kutoka
katika makundi mbalimbali chama hicho kuwa makini kumteua mgombea
anayekubalika, msafi na mwenye kuchagulika ambaye atatoa ushindani kwa
wagombea wa upinzani, hasa Ukawa.
Vilevile, kumekuwapo na wasiwasi wa baadhi ya
wagombea kutishia kukihama chama hicho endapo majina yao yatakatwa,
jambo ambalo pia linakiweka njia panda.
Nape: Hakuna shinikizo
Hata hivyo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM,
Nape Nnauye amejibu hoja hizo akisema chama hicho hakitafanya uamuzi kwa
kushinikizwa na watu, bali kitafuata taratibu na kanuni.
“Tunazo taratibu, tunazo kanuni zetu. Nataka
kuamini kuwa kila mtu aliyegombea anajua kuna kushinda na kuna kushindwa
na kuna kuteuliwa na kutokuteuliwa,” alisema jana alipozungumza na
waandishi wa habari.
Alisema hataki kuamini kuwa kuna mgombea kati ya 38 walioomba nafasi hiyo ambaye anaamini anaingia kushinda tu.
“Usipokuwa wewe anakuwa mwingine... Asiyekubali
kushindwa basi atakuwa si mshindani. Usisahau hizo ni presha za wapambe
hazitupi tabu. Tunachojua walioshindwa watapeana mkono na aliyeshinda na
chama kitabaki kuwa kimoja,” alisema Nape.
Alisema wananchi waamini chama kitatenda haki, taratibu zitafuatwa na kuwapa mgombea bora.
“Haya ni maneno ya presha za barabarani
ninachoamini mwisho wa siku hakuna fujo, hakuna vurugu, vyombo
vimejipanga vizuri hakuna vurugu na wapambe kusindikizana ni jambo la
kawaida,” alisema na kuongeza kuwa anafahamu kuwa wapo watakaohuzunika
kutokana na majina ya watu wao kukatwa lakini hakuna jinsi kwa sababu
kanuni za CCM zinasema Kamati Kuu (CC) itapendekeza majina matano kwa
Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC).
Pia kanuni hizo zinasema NEC itapendekeza majina matatu kwa mkutano mkuu ambao utachagua mmoja.
“Hatuna ujanja, tungeweza kusema wote 38 nendeni lakini kanuni
yetu haituruhusu. Wengi wa wagombea wanajua, kwa sababu hawajaanza
jana,” alisema.
Alipoulizwa kuhusu kuondoka kwa wanachama ambao
wagombea wao au wao wenyewe watakatwa katika mchujo huo, Nape alisema
haoni mwanachama atakayeondoka ndani ya chama hicho... “Simuoni mtu
atakayeondoka, hizi ni kelele za wapambe… Hii ni sehemu ya kutengeneza
presha. Ninachotaka kusema, CCM hatumuoni mtu atakayeondoka na kwa nini
aondoke?” alisema.
Haki ya kukata rufaa
Akizungumzia haki ya mgombea kukata rufaa iwapo
jina lake litakatwa na asiridhike, Nape alisema kanuni ziko kimya
hazisemi kuhusu suala hilo na wala hakuna muda wa kufanya hivyo.
“Katika uchujaji wa majina matano kwenda NEC,
hawatoi sababu kwa nini wamelikata jina,” alisema na kufafanua kuwa
hakuna kikao kinachokilazimisha kikao kingine kusema sababu ya kuyakata
majina ya wagombea.
Alisema kuna watu walihoji kuhusu kukatwa kwa
majina yao katika chaguzi kuu za mwaka 1995 na 2005, kwa kukata rufaa
NEC lakini kesi ilichukua dakika tatu na kumalizika vibaya.
“Huwa nawaambia watu tusisahau kuwa hiki chama
ndicho kiko madarakani, vyanzo vya taarifa zake haviwezi kuwa sawa na
Chadema, CUF na wengine, haiwezekani,” alisema.
Hata hivyo, alisema hatarajii kama kuna mtu
atakayekata rufaa katika mchujo huo, lakini haikatazwi kwa mwanachama
kutoa hoja yake katika kikao chochote.
Mgombea anayeuzika
Baadhi ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa
Zanzibar wameeleza hofu ya CCM kuanguka katika Uchaguzi wa Oktoba iwapo
itashindwa kuteua mgombea anayekubalika ndani na nje ya chama hicho.
Mjumbe Khamis Mbeto Khamis alisema CCM ikishindwa
kupata mgombea anayekubalika na wananchi na ndani ya chama ipo hatari ya
kuandika historia mpya ya kupoteza dola kama ilivyotokea kwa vyama
vilivyopingania ukombozi vya Malawi, Kenya na Zambia.
“Mie sitaki kuwa sehemu ya wajumbe watakaoandika
historia ya CCM kuondoka madarakani katika kipindi cha uongozi wetu,
tuache mizengwe, chuki na uhasama tupate mgombea bora,” alisema Khamisi.
Alisema mgombea ambaye hana msingi wa kisiasa, mvuto na
kukubalika kwa wananchi wa pande mbili za Muungano ni hatari
kumsimamisha kutokana na ushindani mkubwa wa kisiasa unaoendelea
kujitokeza.
Mwenyekiti wa wenyeviti wa mikoa sita ya kichama
ya CCM Zanzibar, Haji Juma Haji alisema CCM inatakiwa izingatie masilahi
ya chama na Taifa kwa kusimamisha mgombea mwenye uwezo wa kukabiliana
na mabadiliko ya hali ya kisiasa.
“Muhimu tuchague anayetakiwa na wananchi, awe
anakubalika na mwenye uwezo wa kuendeleza amani na usalama wa Taifa
letu,” alisema bila kumtaja mgombea huyo.
Mjumbe mwingine, naibu waziri wa zamani wa
Muungano, Dk Maua Daftari aliwataka wajumbe wa vikao vya uteuzi
wazingatie sifa 13 zilizowekwa na chama wakati wa kuwajadili wagombea
ikiwamo ya kumpata mtu anayekubalika.
“Muhimu tusifanye hiana, tuwe wa kweli na tusiweke
chuki katika kutafuta mgombea urais, mazingira ya kisiasa yamebadilika
lazima tuangalie mbele na nyuma, sifa bora za uongozi 13 za chama uwe
msingi wetu wa kupata mgombea,” alisema Dk Daftari.
Mjumbe mwingine, Rashid Ali Juma alisema CCM
inapita katika wakati mgumu hivyo ni lazima apatikane mgombea
anayekubalika kwa wananchi ndani ya chama.
Hofu ya wajumbe wa NEC inajitokeza wakati kesho
wajumbe 123 wa Halmashauri Kuu ya CCM Zanzibar na wengine 213 wa Mkutano
Mkuu wakianza safari kwenda Dodoma kuchagua mgombea urais wa Zanzibar
na Muungano.
Ratiba ya vikao
Jana, kikao cha sekretarieti kilichoongozwa na
Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana kilikaa kikiwa na ajenda moja ya kupitia
maandalizi ya mkutano mkuu ambayo ni pamoja na kuhakiki ratiba, malazi
ya wajumbe, makabrasha na nyaraka mbalimbali zitakazotumika katika vikao
hivyo.
Leo, kutakuwa na kikao cha Kamati ya Maadili na
Usalama kitakachoendeshwa na Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete na
kesho kutakuwa na ufunguzi ukumbi wa chama hicho na baadaye kikao cha
Kamati Kuu (CC) kitakachoteua majina matano ya wanaowania urais.
Kikao cha NEC kitakaa Ijumaa kwa ajili ya
kumdhibitisha mgombea wa urais wa Zanzibar, kupitia Ilani ya Uchaguzi ya
2015 – 2020 na kupigia kura majina matano ambayo yatawasilishwa na CC
kwa ajili ya kutoa majina matatu ya wagombea urais, ambayo yatakwenda
katika Mkutano Mkuu utakaofanyika Jumamosi hadi Jumapili ambao utakuwa
na ajenda mbili, kupitisha Ilani ya Uchaguzi na kupigia kura majina
matatu yaliyopendekezwa na NEC kumpata mgombea urais.
“Napenda kuwahakikishia Watanzania wenzangu kuwa
tumejipanga vizuri, tutatoka tukiwa wamoja na ushindi,” alisema Nape na
kuwahakikishia wajumbe kuwa hakuna atakayekosa malazi.
