Dar es Salaam. Wakati wa hali
ya sintofahamu ikiwa imetawala uteuzi wa mgombea atakayeungwa mkono na
vyama vinne vya upinzani, imebainika kuwa mzozo unaochelewesha suala
hilo ni mgombea ambaye Chadema haijamuweka bayana.
Katibu
wa Chadema, Dk Willibrod Slaa ndiye ambaye anapewa nafasi kubwa ya
kupitishwa kugombea urais kwa tiketi ya Ukawa mbele ya mwenyekiti wa
CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na kada wa NCCR-Mageuzi, Dk George
Kahangwa, lakini hadi sasa vyama hivyo bado vinasita kumtangaza mteule
wake.
Profesa Lipumba alikuwa amewaahidi waandishi wa
habari wiki iliyopita kuwa mgombea ambaye ataungwa mkono na vyama hivyo
vya Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF na NLD angetangazwa Julai 14, lakini siku
hiyo hakuna aliyetangazwa.
Badala yake viongozi wa
Chadema, NLD na NCCR ndio waliofika Hoteli ya Coloseum jijini Dar es
Salaam ambako Profesa Lipumba aliahidi kuwa ndiko jina la mgombea huyo
lingetajwa, wakati viongozi wa CUF hawakuonekana na baadaye jioni
wakasema kuwa walikuwa na kikao cha ndani ya chama cha kutafuta ufumbuzi
wa mambo ambayo walikuwa hawajakubaliana.
Vyama hivyo
vitatu vikaeleza baadaye kuwa jina hilo litatangazwa ndani ya siku saba
kuanzia Julai 14, lakini siku iliyofuata CUF ilisema suala la kuachia
chama kingine jukumu la kusimamisha mgombea urais litawasilishwa kwenye
kikao cha Baraza Kuu la chama hicho ambacho kitafanyika Julai 25, jambo
ambalo lilikubaliwa na vyama hivyo vitatu.
Matamko
hayo yamefanya suala la mgombea urais wa Ukawa kugubikwa na giza nene,
lakini kwa siku tatu Mwananchi imefuatilia na kubaini kuwa mgombea
ambaye yuko na hajatajwa rasmi kwa vyama hivyo vinne ndiye
anayechelewesha mchakato huo na amesababisha kuwapo na hatari ya umoja
huo kuparaganyika.
Habari zilizolifikia gazeti hili
kutoka ndani ya vikao vya Ukawa vilivyoanza kufanyika takribani wiki
mbili jijini Dar es Salaam, zinaeleza kuwa licha ya viongozi wa vyama
hivyo kumpata mgombea wao wa urais katika kikao cha Julai 14 mwaka huu,
walikwama kumtangaza kutokana na CUF kutokuwapo kikaoni ikielezwa kuwa
wanapinga maendeleo ya mchakato huo.
Taarifa hizo
zinaeleza kuwa msimamo huo wa CUF umetokana na utata ulioibuka katika
kikao cha Ukawa cha Julai 11 na 14, baada ya wagombea wawili kati ya
watatu, kukubali mmoja wao agombee urais, lakini chama chake kikasema
kuwa kinachotakiwa ni Ukawa kutangaza jina la chama kitakachotoa mgombea
na si jina la mgombea.
Tayari Profesa Lipumba
ameshachukua fomu za kuwania urais kwa tiketi ya CUF, wakati Dk Kahangwa
amechukua fomu kuwania urais kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi, huku mchakato
wa Chadema ukiwa haujaanza.
Habari hizo zinaeleza kuwa
awali kulikuwa na mvutano mkali kati ya Profesa Lipumba na Dk Slaa na
kwamba katika kikao cha Julai 11, Lipumba ambaye ni mwenyekiti wa CUF
alikubali kumuachia Dk Slaa agombee urais kupitia Ukawa, lakini
inaonekana hata ndani ya Chadema bado hawajaafikiana kuhusu jina la
mgombea.
Hata hivyo, chama hicho kimeeleza kuwa jina la mgombea urais limeshapatikana na linasubiri muda muafaka.
“Tutamtangaza
mgombea urais wa Ukawa ndani ya wiki moja kama tulivyosema awali,”
alisema Naibu Katibu Mkuu wa Chadema-Bara, John Mnyika jana.
“Wananchi wanatakiwa kutulia tu, siku ikifika tutatangaza.”
Mnyika
alitoa ufafanuzi huo muda mfupi baada ya kulieleza gazeti hili jana
kwamba wanaopaswa kuzungumzia suala hilo ni Dk Slaa na Profesa Lipumba.
Jibu
kama hilo la Mnyika lilitolewa pia na mwenyekiti wa NLD, Dk Emmanuel
Makaidi alipoulizwa kuhusu habari kwamba kuna jina la mgombea urais
linalosumbua Ukawa.
“Sijui chochote kuhusu hilo. Ila watu hawa wawili, Mbowe na Dk Slaa watakusaidia kujua kuhusu jambo hilo.”
Alipobanwa
zaidi, alisema: “Unajua hata mimi nazisikia sana habari kama hizo
pamoja na nyingine nyingi. Katika Ukawa watu wanazungumza ndani ya vikao
na nje ya vikao, ila wa kulithibitisha hilo ni hao watu wawili
niliokutajia.”
Lakini mpashaji habari wetu alisema
ugumu wa kumpata mgombea urais wa Ukawa kutoka Chadema unasababishwa na
chama hicho kutotaka kuweka bayana jina la mtu atakayebeba jukumu hilo
wakati wameshakubaliana kuwa Dk Slaa ndiye asimamishwe.
“Inaonekana
kama kuna mtu mwingine hivi. Wote tumekubali mgombea awe Dk Slaa,
lakini Chadema wenyewe wanazuia asitangazwe,” alisema mpashaji huyo
kutoka ndani ya vikao vya Ukawa.
Habari zaidi zinaeleza
kuwa ndani ya Chadema kuna mvutano, kwani wapo wanaotaka Dk Slaa
atangazwe kuwa ndiye mgombea na wanaotaka asitangazwe lakini hawaweki
bayana kuwa hawamtaki au wanataka mtu mwingine.
Hata
hivyo, habari hizo zinasema kuwa sababu nyingine inayochelewesha suala
hilo ni Chadema kutotaka kumtangaza mgombea wake kutokana na mchakato
wake wa uteuzi wa mgombea urais kutoanza. Mchakato huo utaanza Julai 20
na kumalizika Julai 25, siku ambayo CUF itakuwa na kikao chake cha
Baraza Kuu kuamua mgombea urais.
Habari zinasema kuwa
Chadema imekuwa ikisisitiza kuwa Ukawa itaje jina la chama kitakachotoa
mgombea urais na si jina la mwanachama atakayegombea nafasi hiyo.
Habari
hizo zinaeleza kuwa chama hicho kinachoongoza kambi ya upinzani,
kinadai kuwa Ukawa kutangaza jina la mwanachama atakayegombea urais ni
kuingilia mchakato wa Chadema ambao humalizika kwa kikao cha juu
kupitisha mgombea urais wa chama.
Awali baada ya
kuchukua fomu ya kugombea urais kwa tiketi ya CUF, Profesa Lipumba
alikuwa akisema kwenye mikutano ya hadhara kuwa vyama hivyo vinne
vimekubaliana kuwa kila kimoja kifanye mchakato wake wa kupata mgombea.
Alisema kila chama kitalazimika kupeleka Tume ya Uchaguzi (NEC) jina la
mgombea wake ili kiwe na uhakika kuwa amepitishwa halafu ndipo vikutane
na kuamua mmoja atakayeungwa mkono na vyama vyote.
Lakini
hali hiyo ilibadilika mwishoni mwa mchakato wa CCM wa kumpata mteule
wake wa mbio za urais baada ya Ukawa kuitisha mkutano wa pamoja na
wabunge wa vyama vinavyounda umoja huo ambao habari zinasema
walishinikiza kuwa mgombea wa Ukawa atangazwe mapema na si kusubiri
mchakato wa kila chama.
Mvutano ndani ya Ukawa ulianza
wakati CUF ilipotaka iachiwe nafasi ya kusimamisha mgombea urais kwa
madai kuwa Chadema imeshaunda mtandao mzuri na hivyo itakuwa na nafasi
ya kuingiza wabunge wengi, lakini chama hicho kinachoongoza kambi ya
upinzani bungeni kikaeleza kuwa CUF ilishaachiwa nafasi ya kusimamisha
mgombea urais wa Zanzibar.
matukio hayo yanatokea
wakati aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa akiombwa asiondoke CCM
baada ya kuenguliwa kwenye mchakato wa urais wa chama hicho tawala.
Makada
kadhaa wamejitokeza hadharani na kumsihi mbunge huyo wa Monduli
kukubali matokeo na kutofanya uamuzi wa kuondoka, huku watu wanaosema
kuwa wanachama wa CCM wakitangaza kujivua uanachama na kujiunga na
Chadema kwa maelezo kuwa hawakubaliani na uamuzi wa chama hicho tawala
kumuengua Lowassa.
Lowassa hajatoa kauli baada ya
kuenguliwa CCM na mapema wiki hii kulikuwa na habari kuwa angeongea na
waandishi wa habari, lakini mkutano huo ukafutwa saa chache kabla ya
kuanza.
chanzo: mwananchi