Nairobi, Kenya.
Shangwe na shamrashamra zimeendelea kutawala mjini Nairobi kufuatia kuwasili kwa Rais wa Marekani Barack Obama aliyewasili jana akiwa ameambatana na ujumbe mzito.
Rais Obama ambaye alipokewa na mwenyeji wake, Rais Uhuru Kenyatta na
baadaye kuwa na mazungumzo mafupi hii ni ziara yake ya kihistoria na
inafanyika katika wakati taifa la Kenya likijitahidi kujitambulisha upya
baada ya kuandamwa na matukio ya kigaidi na mvutano wa siasa za ndani.

Leo kufungua mkutano wa kibiashara
Rais Obama leo atajitokeza hadharani kwa mara ya kwanza akifungua
mkutano wa kimataifa unawajumuisha wajasiriamali, wachumi pamoja na
wawekezaji mkutano ambao unatajwa kuwa na umuhimu mkubwa kwa uchumi wa
Kenya.
Mkutano huo ambao pia unahudhuria na zaidi ya wajumbe 3,000
unachukuliwa kama daraja muhimu la kuanzisha majadiliano ya uwekezaji
baina ya Marekani na Kenya hasa kupitia mpango unaojulikana kama Agoa.

Akizungumza muda mfupi kabla ya kuanza kwa ziara yake hiyo mjini
Washington, Rais Obama aliitaja Afrika kama bara linalochipua kwa kasi
na linapaswa kuungwa mkono kwa kila hatua.
Hii ni ziara yake ya kwanza tangu aingia madarakani na kwamba
inachukuliwa kama fursa ya pekee kwa Kenya kukuza utalii na kuwavutia
wawekezaji wa kigeni.
Obama kuzungumza na wanafunzi, kuhutubia taifa
Kesho inatarajiwa kuwa moja ya siku yenye shughuli nyingi kwa Rais
Obama ikiwamo kukutana kwa faragha na ndugu na jamaa zake walisafiri
kutoka kijiji alichozaliwa cha Kogelo hadi mjini Nairobi kukutana na
kiongozi huyo.

Pia, Rais Obama atatembelea Chuo Kikuu cha Kenyatta na baadaye
kuzungumza na viongozi vijana akielezea mambo mbalimbali yanayohusu
utawala na kuwapa moyo namna wanavyoweza kutimiza ndoto zao. Baadaye
ataelekea katika Uwanja wa Karasani ambako anatarajia kutoa hutuba yake
inayosubiriwa na wengi.
Jumla ya watu 5,000 ikiwamo wabunge, wawakilishi wa mashirika ya
kiraia, wafanyabiashara na maofisa wa serikali watahudhuria mkutano huo.
Haikuweza kufahamika mara moja yale yatakayojitokeza kwenye hotuba yake
hiyo lakini kuna uwezekano mkubwa akagusia masuala yanayohusu utawala
bora, mapambano dhidi ya ugaidi na vipaumbele vya maendeleo kwa Afrika.

Waziri Kenya aishukia CNN
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya, Joseph Nkaissery ameitaka a
televisheni ya CNN ya Marekani kuwaomba radhi Wakenya kwa kuitaja nchi
hiyo kuwa ni uwanja wa ugaidi.
Waziri Nkaissery amesema: Kama televisheni ya CNN imestaarabika vya
kutosha basi ilipaswa kuwaomba radhi Wakenya. Waziri huyo alisema nchi
hiyo inakabiliwa na mashambulizi ya kigaidi kama zilivyo nchi nyingine
dunia lakini suala hilo haliifanyi kuwa eneo salama kwa ugaidi.
Waziri Mkaisserry amewataka Wakenya kuidharau ripoti ya televisheni
ya CNN kama inavyostahiki. Msimamo huo mkali wa Kenya umekuja baada ya
kituo cha televisheni ya CNN cha Marekani kupeperusha habari iliyodai
kuwa Kenya ni ‘uwanja wa ugaidi’, siku moja kabla ya Rais wa Marekani
kuwasili nchini humo.
CNN ilipeperusha habari iliyodai, “Rais Barack Obama siyo tu anaenda nyumbani kwa babake, pia anazuru ‘uwanja wa ugaidi.”
(CREDIT: MWANANCHI)
(CREDIT: MWANANCHI)