
Katibu wa NEC-CCM
Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye akizungumza
mapema leo jijini Dar na Waandishi wa habari, alieleza kuwa wataondoka jijini Dar kesho kwa basi
maalumu, ambapo watasimama njiani katika mikoa ya Morogoro, Dodoma,
Singida na mengineyo kwa ajili ya kusalimia wananchi.

Katibu wa NEC-CCM
Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye akisisitiza jambo zaidi kwa Waandishi wa habari, kuhusiana na ziara hiyo itakayoanza kesho.
KATIBU
Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana anatarajia kuanza
ziara ya siku 28 kesho katika mikoa mitatu ya Kagera, Geita na Mwanza
kukamilisha mikoa yote 30 nchi nzima.
Ziara
hizo zenye malengo ya kukagua utekelezwaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM
mwaka 2010 na kuimarisha chama zimekuwa na mafanikio kwa kuondoa
matatizo mbalimbali yanayowakumba wananchi hasa wa mikoani.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar leo, Katibu wa NEC-CCM Itikadi na
Uenezi, Nape Nnauye alisema wataondoka jijini Dar kesho asubuhi kwa basi
maalumu, ambapo watasimama njiani katika mikoa ya Morogoro, Dodoma,
Singida na mengineyo kwa ajili ya kusalimia wananchi.
“Ziara
rasmi itaanza June 4 katika Wilaya ya Nyakanazi mkoani Kagera, lakini
kesho tutakunywa chai Morogoro chakula cha mchana tutakula Dodoma halafu
tutasalimia wananchi katika Mikoa ya njiani kama Singida, Nzega na
tumepanga kulala Kahama mkoani Shinyanga, tukiamka ziara ndio itaanza
rasmi,” alisema Nape.
Aliongeza
kuwa katika ziara hiyo watatembelea majimbo yote ya uchaguzi hivyo
amewataka wana-CCM na wananchi wengine kujitokeza kwa wingi kumsikiliza
Katibu Mkuu katika ziara hiyo ya kihistoria.
“Hii
ni ziara ya kihistoria kwa sababu ya mambo matatu, kwanza tutatembelea
visiwa vyote vya Ukerewe ambavyo ni nadra kutembelewa na viongozi, pili
huu ni mwaka wa uchaguzi kuna masuala mengi yanahitaji ufafanuzi,”
alisema.
Akitaja
ratiba ya ziara hiyo Nape alifafanua kuwa, “Kuanzia Juni 5 mpaka Juni
15 tutakuwa Mkoa wa Kagera, Juni 16 mpaka 21 tutakuwa Mkoa wa Geita na
Juni 22 mapaka Julai 2 tutakuwa Mwanza kuhitimisha ziara ya nchi nzima
kwa mkutano mkubwa wa kihistoria.”
Akijibu
maswali ya waandishi wa habari kuhusu faida za ziara hizi Nape alisema
kuna masuala mengi ya kimaendeleo yalisimama lakini alipopita Katibu
Mkuu Kinana ufumbuzi umepaikana, akitolea mfano mashamba
yaliyobinafsishwa bila kufuata utaratibu alisema Rais Jakaya Kikwete,
amefuta hati nyingi za mashamba ya wawekezaji na kurudishwa kwa
wananchi.
“Kuna
baadhi ya maeneo kulikuwa na zahanati zimeshajengwa lakini hakuna
vibali, nimepata taarifa kuwa vibali vimeshapatikana na huduma
zinaendelea, kulikuwa na matatizo ya ardhi za wananchi kuchukuliwa na
wawekezaji katika maeneo ya Tanga, Arusha, Babati na maeneo mengine
lakini kila kitu kipo sawa sasa na wananchi wanamshukuru Kinana,”
alisema.
Aliongeza
kuwa, “Nisisitize kuwa tumesema tutaondoka na basi maalumu kwa sababu
kama kuna mwingine atafanya hivyo atakuwa ametuiga, mkumbuke hili wazo
la kuondoka na basi ni la Katibu Mkuu.”.
Ikiwa
ziara hizi zitamalizika salama Julai 2 mwaka huu, Kinana atakuwa Katibu
Mkuu pekee wa CCM tangu kuanzishwa kwake Februari 5, 1977 kuzunguka
nchi nzima kuangalia uhai wa chama na kusikiliza na kutatua kero za
wananchi wote bila kujali itikadi za vyama.