Waziri mkuu Mstaafu Fedrick Sumaye.
Wakati tafrani hiyo ikitokea mjini Mbeya, Balozi Amina Salum Ali alisema mjini Tanga kuwa hajawahi kuona nchi ambayo mtu anaiba fedha, halafu anaambiwa azirejeshe bila ya kuchukuliwa hatua zozote, akisema huo ni udhaifu mkubwa katika kudhibiti ufisadi.Kazi ya Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye ya kusaka wadhamini juzi nusura iingie dosari baada ya wanachama kutaka kuchana fomu zenye orodha ya wadhamini kwa madai kuwa hawakupewa “nauli” ya kwenda ofisi za CCM kufanya kazi hiyo.
Wakati tafrani hiyo ikitokea mjini Mbeya, Balozi
Amina Salum Ali alisema mjini Tanga kuwa hajawahi kuona nchi ambayo mtu
anaiba fedha, halafu anaambiwa azirejeshe bila ya kuchukuliwa hatua
zozote, akisema huo ni udhaifu mkubwa katika kudhibiti ufisadi.
Katika sakata la Mbeya, kundi la baadhi ya
wanachama kutoka kata nne waliokabidhi kadi na kuandikwa majina yao
kwenye ofisi za CCM za Wilaya ya Mbeya Mjini, liliambiwa kuwa hakukuwapo
na posho kwa ajili ya kazi hiyo.
Kauli hiyo ilisababisha wanachama hao kupora na kutaka kuchana fomu iliyokuwa na majina yao.
Katibu wa CCM wilaya hiyo, Kulwa Milonge alisema
tukio hilo lilikuwa kubwa na kuhatarisha usalama, lakini chama
kiliingilia kati na kusawazisha mambo.
Milonge alisema hadi mwisho wa tukio hilo, ofisa aliyetumwa na Sumaye kukusanya saini hizo aliondoka na majina 45 ya wadhamini.
Sumaye ni mmoja kati ya wanachama wengi
waliojinadi kuwa wanachukia rushwa na ameeleza bayana kuwa iwapo CCM
itampitisha mlarushwa, atajiondoa.
Balozi Amina aikomalia rushwa
Mkoani Tanga, Balozi Amina alisema kwa kutumia
uzoefu wake kimataifa katika masuala ya fedha, amebaini kuwa kuna tatizo
la kushindwa kudhibiti ufisadi uliokithiri nchini.
“Sijapata kusikia nchi yoyote duniani mtu
anapatikana na hatia ya kufanya ubadhilifu mkubwa wa fedha za umma,
halafu anaambiwa tu arejeshe na hakuna hatua anazochukuliwa,” alisema
Balozi Amina.
Alisema iwapo atapewa fursa ya kuwa Rais wa
Serikali ya Awamu ya Tano, atatumia nguvu kubwa kupambana na ufisadi
unaorutubishwa na tabia ya kulindana kwa sababu hata kama kutakuwa na
uzalishaji mkubwa, kama kuna mifereji ya rushwa, uchumi hauwezi kukua.
Alisema Tanga ina uwezo wa kubadilika na kuwa
kitovu cha uchumi wa Tanzania nzima iwapo Bandari ya Tanga itaboreshwa
kwa kujengwa ya Mwambani na reli ya Tanga-Arusha-Musoma hadi Uganda.
Wingi wamtisha Pinda
Wakati mwakilishi wa Sumaye akipata matatizo hayo,
hali ilikuwa tofauti kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambaye alikuwa
ofisi ya CCM ya Mbeya Vijijini kusaka wadhamini.
Waziri Pinda alisema mbele ya wanachama
waliojitokeza kumdhamini kuwa mwili wake unasisimka na kujaa hofu kwa
jinsi wanachama wengi wanavyozidi kujitokeza kuomba urais. Alisema
anatishwa zaidi na mitazamo ya baadhi ya wagombea ambao wanaonekana
kuitaka dhamana hiyo kwa nguvu zote.
Lakini akasema anatiwa nguvu na idadi kubwa ya
wanachama wanaomuunga mkono na kwamba anazidi kusonga mbele akimtumaini
Mungu kwamba akipenda atafanikiwa.
“Nawaomba mtuombee wote tuliojitokeza kusaka urais ili apatikane mmoja ambaye itabidi aungwe mkono na wengine wote,” alisema.
Alisema wapo baadhi ya wagombea ambao wanaonekana
kana kwamba hawatakubali matokeo watapokataliwa na jambo hilo linaweza
kuleta mtikisiko ndani ya chama.
Lowassa adhaminiwa na maelfu
Mkoani Mtwara, zaidi ya wanachama 3,500
walijitokeza katika ofisi za chama hicho za wilaya kwa ajili ya
kumdhamini Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.
“Mapokezi ya leo ni historia kubwa kwangu na CCM,
nawashukuru sana kwa sababu tangu nije Mtwara hii haijawahi kutokea na
imani huzaa imani. Hapa mmenipa Imani,” alisema Lowassa.
Alieleza sababu za kugombea akisema: “nimechoshwa na umaskini, lazima tufanye maarifa kwa uwepo wawekezaji kutoka nje.”
“Msiichezee bahati ya gesi, uwepo wa kiwanda cha
saruji, mbolea na vinginevyo vitakavyokuja, vyote vimeshuka kwa bakuli
la neema na neema hii itaendelea kuwapo kama amani itaendelea kuwapo,”
alisema.
Habari hii imeandikwa na Sadi Makomba, Silyvester Mkombe, Burhani Yakub, Justa Mussa, Godfrey Kahango na Haika Kimaro.
chanzo: MWANANCHI
chanzo: MWANANCHI
