Na Bashir Yakub.
Mara
nyingi nimeandika kuhusu ardhi hususan viwanja na nyumba.
Katika kufanya hivyo mara kadhaa nimejaribu kuwatahadharisha
watu namna mbalimbali ya kisheria ya kuepuka kuingia katika
migogoro ya viwanja na nyumba hasa wakati wa kununua(
wanunuzi).
Nimewahi
kueleza namna au vitu vya msingi ambavyo hutakiwa kuwa katika
mkataba wa ununuzi wa nyumba au kiwanja. Nikaeleza umuhimu wa
kila kimoja na nikasisitiza kuwa atayekuwa amenunua ardhi na
mkataba wake ukajaaliwa kuwa na vitu hivyo basi si tu
atakuwa amefanya manunuzi bora lakini pia atakuwa amefanya
manunuzi yanayokubalika kisheria.
Ifike
hatua watu waelewe kuwa migogoro mingi ya ardhi huanzia na
kutokuwa makini kwenye manunuzi. Kutokupata ushauri wa kisheria
ikiwa ni pamoja na kutopitia hatua za msingi za kisheria kabla
ya manunuzi, kuandikiwa mikataba ya manunuzi isiyokidhi vigezo
vya kisheria ikiwemo ile ya serikali za mitaa ambayo
hairuhusiwi kabisa kisheria ni kati ya sababu chache kati ya
nyingi zitakazokupelekea uingie katika mgogoro. Leo nitaeleza
hatua moja ya msingi sana ambayo hutakiwi ufanye manunuzi ya
ardhi bila kuipitia.
1.HATUA TANO ZA KUFUATA UNUNUAPO NYUMBA/KIWANJA.
Ziko
hatua tano muhimu za kupitia pale unapo kuwa katika mchakato
wa kununua ardhi. Umuhimu wa hatua hizi ni kuwa kwanza
kabisa si rahisi kujikuta katika mgogoro unapokuwa umezipitia.
Lakini pili hata bahati mbaya utokee mgogoro basi wewe
uliyepitia hatua hizo utakuwa salama na kama ni kesi basi
wewe upo katika mazingira mazuri ya kushinda. Hatua ya kwanza
huitwa hatua kabla ya mkataba( pre contractual stage).
Hatua
hii inayo mambo yake ya msingi na ya kisheria ambayo
kuyafuata kwako kwaweza kukuweka mbali na hatari ya kununua
ardhi yenye mgogoro au itayokuingiza katika mgogoro . Hatua hii
ndiyo nitakayoeleza kama msingi wa makala ya leo kama
tutakavyoona. Kabla ya kueleza hatua hiyo ni vema pia
nikazitaja hatua nyingine japo kwa ufupi. Hatua ya pili huitwa
hatua ya mkataba( contractual stage). Hii ni hatua ya kupitia
na kujiridhisha na mkataba wa manunuzi ikiwa ni pamoja na
kuusaini. Hatua ya tatu huitwa “pre completion stage”, hatua ya
nne huitwa hatua ya kumalizia ( completion stage) na hatua ya
tano na ya mwisho huitwa hatua baada ya kumalizia ( post
completion stage).
