BASATA YALAANI TABIA CHAFU NA ISIYO NA MAADILI ILIYOONESHWA NA MSANII SHILOLE KWENYE ONESHO LAKE NCHINI UBELIGIJI.
Katika picha hizo
ambazo zimelaaniwa na watanzania wengi nchini kupitia njia mbalimbali ikiwemo
mitandao ya kijamii, Shilole anaonekana akiwa Jukwaani huku viungo vyake vya sehemu
za siri vikiwa hadharani na zaidi akionesha tabia ambazo kwa kiasi kikubwa
zimefedhehesha na kuidhalilisha sekta ya Sanaa na Taifa kwa ujumla.
Aidha, BASATA
limepokea malalamiko kwa njia ya simu na mawasiliano ya internet kutoka kwa
watanzania waishio ughaibuni wakilaani tukio la Msanii huyo. Katika mawasiliano
yao wameeleza kwamba wamefedheheshwa na kudhalilika na tabia hiyo chafu
iliyooneshwa na msanii huyu.
Ikumbukwe kwamba,
Shilole ni msanii aliyesajiliwa na Baraza la Sanaa la Taifa, hivyo anapokwenda
nje ya nchi kabla hajapata visa anapewa barua ya utambulisho kama msanii wa
Tanzania, hivyo anapokuwa nje ya nchi anatambuliwa kama msanii Mtanzania,
anapofanya kinyume na misingi ya kazi ya Sanaa, anajifedhehesha yeye mwenyewe,
kazi ya Sanaa na nchi yetu pia.
Aidha, ikumbukwe
kwamba BASATA limeshapata kumwita na kumuonya msanii huyu kutokana na tabia
yake ya kutokujiheshimu pale awapo jukwaani na yeye aliahidi kubadilika na
kuachana na tabia hiyo chafu. Kwa hiyo kuendelea kwake kufanya matukio hayo na
kwa sasa katika ardhi ya nchi nyingine ni uthibitisho kwamba hajabadilika na
kwa maana hiyo ameendelea kuidhalilisha Sanaa na wasanii wa kitanzania wenye
kujitambua na kuiheshimu Sanaa kama kazi nyingine.
BASATA linapenda kueleza kwamba;
1. Litamuita kwa mara nyingine tena kumtaka ajieleze kwa nini alifanya onesho hilo la kujidhalilisha na kudhalilisha hadhi ya mwanamke, msanii na Sanaa kwa ujumla2. Kama maelezo yake hayataridhisha hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake maana tayari ameshadhihirisha kwamba akifanyacho si Sanaa na hakina uhusiano na kazi ya Sanaa ambayo ina heshima yake na inahitaji ubunifu, weledi na kujitambua
BASATA
linawakumbusha wasanii wote nchini kuwa Sanaa ni kazi kama kazi zingine lakini
siku za hivi karibuni wasanii wengi wamekuwa wakikiuka suala zima la maadili
kwa kutengeneza kazi chafu zisizofaa mbele ya jamii ya watanzania wanaoipenda
na kuiheshimu kazi ya Sanaa yenye staha. Tuungane kwa pamoja kukemea kazi chafu
zinazozalishwa na wasanii wasiojitambua kwani suala la maadili ni suala
mtambuka na linaanzia katika ngazi ya familia.
Aidha, BASATA linawataka Wasanii wote nchini kufuata sheria, kanuni na taratibu mara wanapopata mialiko ya kikazi kwenda nje ya nchi. Linawakumbusha kwamba haiwezekani msanii kutumia picha chafu na mavazi dhalili na kuonyesha utupu katika kuvuta mashabiki.
Sanaa ni kazi,
tuipende na kuithamini
Godfrey MngerezaKATIBU MTENDAJI.