Katika
picha hii ya Maktaba, Amiri Jeshi Mkuu , Rais Jakaya Mrisho Kikwete
akimtunuku nishani ya kumbukumbu ya miaka 50 ya Jeshi la Wananchi wa
Tanzani ( JWTZ) Brigedia Jenerali Sara Thomas Rwambali ambaye hivi
karibuni, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Dr. Nkosazana
Dlamini Zuma amemteua kuwa Mwakilishi Maalum na Mkuu wa Ofisi ya Umoja
wa Afrika nchi Sudani ya Kusini.
Na Mwandishi Maalum, New York
Mwenyekiti
wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Dr. Nkosanzana Dlamini Zuma,
amemteua, Brigedia Jenerali Sara Thomas Rwambali kutoka Jeshi la
Wananchi wa Tanzania ( JWTZ),kuwa Mwakilishi Maalum na Mkuu wa Ofisi
ya Umoja wa Afrika Sudan ya Kusini .
Kwa
mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na AU na nakala
yake kutumwa Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa,
inaeleza kwamba makazi ya Brigedia Jenerali Sara Thomas Rwambali
yatakuwa Juba.
Pamoja
na uteuzi wa Brigedia Jenerali Sara Rwambali, Dr. Nkosazana Dlamini
Zuma pia amewateua Madame Josephine- Charlotte Mayuma Kala kutoka
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, anayekuwa Mwakilishi Maalum na Mkuu
wa Ofisi ya Umoja wa Afrika huko Cote d’Ivoire na makazi yake yakiwa
Abidjan,
Wengine
walioteuliwa ni Madame Nyiramatama kutoka Rwanda, anayekuwa Mkuu
wa Ofisi ya AU huko Chad , makazi yake yakiwa Ndjamena na Dr. Arvin
Boolel kutoka Mauritius anayekuwa Mwakilishi Maalum na Mkuu wa Ofisi
ya AU katika Maziwa Makuu Burundi na makazi yake yakiwa Bujumbura.
Taarifa
kwa vyombo vya Habari kutoka AU inaeleza zaidi kwamba uteuzi huo ni
sehemu ya AU ya kuhakikisha uwepo wake katika kila eneo na vile vile
kuunga mkono juhudi zinazolenga katika kukuza Amani na Usalama
Barani Afrika
“Ninatoa pongezi zake za dhati kwa wateuliwa ambao ni viongozi wa ngazi
za juu na wenye sifa za kutukuka katika utumishi wa umma wakiwa na
uzoefu mkubwa katika eneo la amani na usalama. Si jambo la ajabu
kwamba wateule watatu kati ya wanne ni wanawake” anasema Dr. Zuma
Na kuongeza, “katika mwaka huu wa 2015, ambao Umoja wa Afrika umejikita katika uwezeshwaji wa wanawake.
"Ninayo
matumaini makubwa kwamba AU na Afrika kwa ujumla itanufaika na
utaalamu na uzoefu mkubwa na uwezo wa kiuongozi kutoka kwa wateuliwa
hawa”.
Mwenyekiti
wa Kamishna ya AU pia ametoa wito kwa wadau wote kuwapatia
ushirikiano wateuliwa hao ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa
ukamilifu kwa maslahi ya Bara la Afrika, huku akitoa shukrani kwa
wawakilishi ambao wanamaliza muda wao.
