Feb 26, 2015

Hapa na Pale: Chuchu Azirai Ndani ya Jeneza!

Chuchu Hans amejikuta akizirai ndani ya jeneza wakati akiigiza sini ya kifo kwenye filamu. Chuchu alikumbwa na hali hiyo hivi karibuni akiwa ‘lokesheni’ ya kuigizia filamu hiyo maeneo ya Mbezi ya Kimara jijini Dar es Salaam ambapo sanjari na yeye, msanii mwingine aliyecheza nafasi ya mwanakwaya naye alipoteza fahamu wakati kipande hicho kikirekodiwa.
Chanzo kimoja kutoka ndani ya kundi la wasanii waliokuwa wakiigiza filamu kililiambia Gazeti la Amani  kuwa, Chuchu alikumbwa na hali hiyo kutokana na wasiwasi na ujasiri wa kuuvaa uhusika.
“Awali, Chuchu alionesha wasiwasi wa kuigiza kipande hicho cha kumwonesha yeye yumo ndani ya jeneza akiwa amefariki dunia kwa ugonjwa kama wa kichaa kilichotokana na msongo wa mawazo baada ya kubakwa.



“Mbaya zaidi, mwongozaji naye alisema ni lazima akiwa amelala ndani ya jeneza awekewe pamba za kuziba matundu ya pua kama maiti wanavyowekewa,” kilisema chanzo.
Chanzo kikazidi kudai kwamba, taharuki yote hiyo ilitokea pale, ‘mwili’ wa Chuchu ukiagwa kwenye Kanisa la Sabato, Mbezi, Dar ambapo waombolezaji walipokuwa wakipita, binti yake, Farha (9) aliangua kilio kilichomfanya Chuchu ajikute akikata pumzi ghafla!

Ikaelezwa kwamba, ilikuwa wakati kipande hicho kimeisha huku binti yake akiendelea kulia kwa kumwona mama yake ndani ya jeneza, Chuchu hakuamka ili kuendelea na vipande vingine hali iliyowafanya watu wazima kumkagua na kugundua alizirai.

“Watu walianza kupagawa, wengine walijua ameshapoteza maisha. Lakini Mungu mkubwa Chuchu akazinduka na kumkuta mwanaye bado akilia kwa nguvu. Ilibidi wasanii wengine waingilie kati kumtuliza,” kilisema chanzo.
Wakati Chuchu ‘akifufuka’, yule msanii aliyeigiza nafasi ya mwanakwaya yeye alikuwa bado chini amelala chali akiwa hajitambui kwa kile kilichokuwa kikiendelea.“Yule mwenzake ilibidi aitwe mchungaji wa kanisa hilo ambaye alikuwa jirani kwa ajili ya kumwombea japo mchungaji wa filamu hiyo alikuwa ni msanii Jimy Mafufu,” kilisema chanzo.
Gazeti la Amani  limtafuta Chuchu kwa njia ya simu yake ya mkononi na kumuuliza ambapo alikiri kutokea kwa tukio hilo.
  “Yaani siwezi kueleza juu ya ile filamu maana ilikuwa ni hatari tupu na sijui hata mama yangu akiiona itakuaje kwa kweli.
“Lakini kwenye ile sini yangu ndiyo ilikuwa ikihitaji hivyo, nilale kama maiti kweli na huwezi amini lilichimbwa hadi kaburi la ukweli. Mimi nilizimia si chini ya  mara moja. Pumzi yangu ilikata hasa nilipomsikia mwanangu akilia.” Chuchu alieleza.
Jionee hapo juu baadhi ya picha zitakazoonekana kwenye filamu hiyo

Picha habari na BONGO MOVIES.COM