Mwigizaji na mwongozaji mkongwe wa filamu za Kibongo Jacob Stephen
‘JB’ ametoa dukuduku lake la moyoni na kusema kwamba tasnia ya filamu
ipo katika hali mbaya.
JB ambaye amefanya kazi kubwa katika kuiinua tasnia hiyo alisema,
filamu inaangukia katika kifo kama ulivyoanguka muziki wa Bongo Fleva
kutokana na soko kushikiliwa na maharamia.
Staa huyo alisema hali hiyo inawafanya wasambazaji kuanza kuikimbia tasnia hiyo na wengine kushusha bei ya filamu.
“Hali ya soko kwa sasa ni mbaya sana kwani uharamia umezidi, kwa
mtazamo wangu najua tunaelekea mwisho, hata kitendo cha msambazaji
mkubwa kama Steps kuamua kushusha bei ni kutapata na kujaribu kukuruka
kutokana na hali ilivyozidi kuwa mbaya.
“Wasambazaji wa muziki walikuwa wakiwalalamikia maharamia kwa
kuwazidi nguvu na serikali ikabaki kimya bila ya kuyafanyia kazi
malalamiko yao, kama inavyofanyika katika filamu sasa,” aliongeza.
Katika mtazmo wake, JB anaamini kwamba suala la kushusha bei ya
filamu wakati maisha yanapanda ni kifo cha tasnia hiyo inayopendwa na
Watanzania wengi.