Nov 3, 2014

NINI CHA KUFANYA WAZAZI, NDUGU WANAPOMCHUKIA UMPENDAYE?-2

Tuliangalia mfano wa jinsi mwanaume mmoja ambaye yupo ndani ya ndoa kwa kipindi cha miaka kumi, alivyokuwa kwenye mgogoro mkubwa baada ya mke wake wa ndoa kutokea kuwachukia na kuwadharau mno wazazi wa mwanaume kwa sababu ambazo anazijua mwenyewe.

Wazazi nao wakaja juu na kumwambia achague moja, mke au wazazi na kujikuta akishindwa kuamua. Leo tunaendelea kueleza nini cha kufanya unapotokewa na hali kama iliyomkuta ndugu yetu huyo.
NINI CHA KUFANYA?
1. TAFUTA CHANZO CHA TATIZO
Kama nilivyoeleza wiki iliyopita, hatua ya kwanza unayotakiwa kuifanya, ni kutafuta chanzo cha tatizo. Kwa nini mke/mume awachukie wazazi wako? Na kwa nini pia wazazi au ndugu wamchukie mume/mke wako? Lazima kuna sababu kwani hakuna chuki ambayo huwa haina chanzo.
Ukichunguza utagundua kuwa kuna jambo lililosababisha hayo yote, huenda ni kwa sababu wazazi wako walikuwa wanampenda mtu mwingine uliyewahi kuwa naye kwenye uhusiano wa kimapenzi. Au pengine mwenzi wako anawatuhumu wazazi wako kwamba wanashirikiana na wewe kuandaa njama za kumuondoa ili aje mtu mwingine au kuna tuhuma za ushirikina kati ya pande hizo mbili.
Ukishakijua chanzo, utakuwa kwenye nafasi nzuri ya kutatua tatizo.
2. ZUNGUMZA NA KILA UPANDE
Baada ya kukijua chanzo, anza kuzungumza na mwenzi wako, mueleze jinsi unavyojisikia vibaya kutokana na uhasama uliopo kati yake na wazazi wako. Tumia lugha ya upole na muulize anataka nini kifanyike ili chuki yake iishe.
Kama anataka umuoneshe upendo wa dhati, nadhani hilo litakuwa ndani ya uwezo wako, muahidi kwamba kama wewe ndiyo chanzo, utabadilika kwa lengo la kumaliza matatizo. Hata ikibidi, mpe zawadi ambazo zitamfurahisha na kumfanya alegeze msimamo wake