
KAMATI ya Bunge inayoshughulikia Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imeishauri Serikali kuifuta Halmashauri ya Jiji la Mwanza baada ya kubaini upotevu wa zaidi ya Sh bilioni 40.
Mwenyekiti
wa Kamati hiyo, Rajab Mohammed Mbarouk alishauri hayo jana wakati wa
kikao cha kupitia taarifa ya CAG ambapo alisema ubadhirifu huo ni wa
kati ya mwaka 2010 hadi 2013.
Alisema
hesabu za miaka hiyo ndizo zenye matatizo ambapo watendaji wengine
waliopo madarakani wamepandishwa vyeo, lakini wanahusishwa na sakata
hilo.
“Haiwezekani halmashauri kama hii kufanya ubadhirifu wa Sh bilioni 40 bila ya kushirikiana na Serikali Kuu,” alisema.
Kwa
mujibu wa matokeo ya ukaguzi wa CAG, Halmashauri ya Jiji la Mwanza
haikufanya vizuri katika maeneo ya uwekaji wa kumbukumbu za hesabu zake,
udhibiti wa matumizi ya fedha za Serikali na miradi maendeleo.
Aliongeza
kuwa, licha ya halmashauri za mkoa wa Mwanza kupata hati
zisizoridhisha, lakini ya Jiji pekee ndiyo iliyopata hati chafu.
Kwa
upande wake, Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza, Stanslaus Mabula alisema
hawezi kukubali ama kukataa juu ya ubadhirifu huo na kuhoji kuwa bajeti
ya halmashauri ni Sh bilioni 6 na kuwa ubadhirifu wa Sh bilioni 40 ni
kiasi kikubwa cha fedha.
Akizungumzia
kufutwa kwa halmashauri ya Jiji na kuwa Manispaa, alisema si sawa kwani
kuwa Jiji ni kutoa wigo mpana wa maendeleo kwa wananchi na kuwa
wameshapita hadhi ya kuwa Manispaa.
Naye
Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Khalifa Hidda alisema hatokubali kuona
hali hiyo ikiendelea na kwamba atachukua hatua na tahadhari zote.
Miongoni
mwa fedha zinazodaiwa kutafunwa na Halmashauri ya Jiji ni pamoja na Sh
bilioni 1.8 zilizotolewa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi za Jamii (NSSF)
kwa ajili ya malipo ya fidia ya viwanja katika eneo la Bugarika ambapo
halmashauri ilizifungulia akaunti bila kibali cha Serikali.
CHANZO MPEKUZI HURU.COM