
Msanii wa Muziki wa Bongo Fleva a.k.a Rais wa Manzese, Hamad
Ally ‘Madee’ hivi karibuni alilala katika Kituo cha Polisi cha Kigamboni,
Dar akihusishwa na utekaji wa dereva wa
bodaboda, Suedi Waziri (pichani) kisha kumpa kipigo ambapo inadaiwa alisoteshwa
kinomanoma.
Baada ya tukio hilo lililotokea mwishoni mwa wiki iliyopita,
Ijumaa lilinasa picha zinazomuonyesha msanii huyo akihenyeshwa kituoni hapo
huku mmoja wa watu wanaoishi karibu na eneo hilo akinyetisha kuwa, licha ya
ustaa wake Madee alikiona cha mtemakuni.

“Mimi nilikuwepo pale kituoni, nilimshuhudia akiwa amepigwa
pingu huku polisi kama sita hivi, mmoja akiwa na silaha wakiwa wamemuweka chini
ya ulinzi wakimpeleka mahakamani.“Alionekana aliyechoka sana huku akiwa na hofu
ila inavyodaiwa baadhi ya watu wake wa karibu walikuwa wakihaha kumnusuru baada
ya kulala selo,” kilidai chanzo hicho.
Majeraha ya mguuni aliyopata Suedi Waziri baada ya
kushambuliwa na Madee.
Kufuatia msala huo, msanii huyo alipandishwa kizimbani
katika Mahakama ya Kigamboni na baadaye kuwekewa dhamana na baba yake ambapo
kesi yake itatajwa tena Oktoba 6, mwaka huu.
Madee anadaiwa kumteka Suedi na kwenda kumsulubu nyumbani
kwake Manzese baada ya kijana aliyekuwa amepakia kwenye bodaboda yake kukwapua
simu ya msanii huyo na kukimbia.
Katika kushinikiza simu yake irudishwe ndipo Madee
alipomtaiti Suedi na mwisho wa siku akaishia mikononi mwa polisi kwa
kufunguliwa kesi iliyosomeka: VJB/RB/625/2014 KUTEKWA KWA BINADAMU
Imeandikwa na Mayasa Mariwata, Shani Ramadhani na Rhoda Josiah.