HAKUNA lugha nyingine ya kusema zaidi ya kuainisha kuwa pepo wa ajali za barabarani zinazoua mamia ya watu ni uzembe wa kutisha unaofanywa na madereva katika uendeshaji magari bila utii wa sheria. Uchunguzi wa Gazeti la Ijumaa uliofanywa hivi karibuni katika maeneo mbalimbali nchini umebaini kuwa, mbali na mwendo kasi unaotajwa mara kwa mara kuwa unachangia ajali, suala la kutozingatia sheria za usalama barabarani ni hatari zaidi
.
Picha za magari ya abiria yaendayo mikoani zilizotumika ukurasa wa nyuma wa gazeti hili ni kielelezo tosha kuwa madereva wengi hawajui sheria za usalama barabarani au wanazivunja makusudi jambo ambalo husababisha kutokea kwa ajali nyingi za magari kugongana uso kwa uso.
Uamuzi wa kizembe kama huo na ule unaonekana katika picha zilizobeba habari hii ambapo madereva wa magari husika wanaonekana ‘kuovateki’ kinyume cha muongozo wa uendeshaji.Sheria zinamkataza dereva kulipita gari jingine kwenye mlima, mteremko mkali na mahali penye kona, lakini kwa mshangao madereva wengi wamekuwa hawazingatii hilo.
Mbali na ulevi baadhi ya madereva wa mabasi yaendayo mkoani wamekuwa wakiendesha kwa mashindano ya kuwahi kufika waendeko ili wasifiwe na abiria kuwa wamewawahisha jambo ambalo mwishowe kuwahi huko huwatokea puani na kuwasababishia ajali.Taarifa ya polisi inaonesha kwamba kwa mwaka jana pekee kulikuwa na ajali 23,842, kati ya hizo ni za mabasi 931, zilizoua watu 313.